Na. Damian Kunambi, Njombe.
Mkuu wa wilaya ya Ludewa Bi. Victoria Mwanziva amekagua miradi saba (7) ya maji inayo tekelezwa wilayani humo yenye thamani ya Tsh. 13,866,290,252.86 ambayo Kukamilika kwake itaenda kuongeza kiwango cha upatikanaji wa huduma ya maji kutoka asimia 74.3% hadi asilimia 79.7 kwa wakazi wa vijijini na asimia 100% kwa wakazi wa mji wa Ludewa.
Akiwa katika ukaguzi wa miradi hiyo katika maeneo mbalimbali Bi. Mwanziva amewataka viongozi wa ngazi ya kata na vijiji pamoja na wataalamu wa sekata ya maji wilayani humo kuhakikisha wanatembelea miradi ya maji inayotekelezwa wilayani humo ili kuhakikisha miradi hiyo inatekelezwa kwa kiwango stahiki kulingana na fedha zinazoletwa na serikali.
Amesema ziara hiyo imelenga kuhakikisha kuwa wanaLudewa wanapata huduma ya Maji bora, safi, salama na yenye kutosheleza Sambamba na kuonesha kazi kubwa inayofanywa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika sekta ya maji wilayani humo hivyo viongozi na wataalamu pia wanapaswa kuunga mkono juhudi za Rais kwa kuikagua miradi hiyo kwa kufika eneo la mradi badala ya kukagua miradi kwa kupiga simu.
” Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan amedhamiria kumtua mama ndoo kichwani hivyo ili miradi hii iwe bora na kudumu kwa muda mrefu viongozi wetu na wataalamu wanapaswa kuikagua hatua kwa hatua ili kubaini mapema kasoro zilizopo kabla mradi kukamilika badala ya kusubiri mradi ukamilike kitu ambacho kitaitia hasara serikali na kuufanya mradi huo kutokuwa bora”. Amesema Bi. Mwanziva.
Hata hivyo kwa upande wake Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya hiyo Sunday Deogratius alisema wameweka sheria ndogo ya utunzaji miradi ya maji na vyanzo vyake ambapo mtu yeyote atakayebainika kufanya uharibifu wowote atachuliwa hatua kali kisheria huku Meneja wa Mamlaka ya maji vijijini (RUWASA) Eng. Jeremiah Maduhu akisema tayari wameunda jumuiya mbalimbali ambazo zitakuwa zikisimamia na kulinda miradi hiyo na vyanzo vyake.
Mkuu huyo wa wilaya amefika katika miradi iliyopo katika kata ya Miradi Mavanga, Ludewa, Iwela, Manda na kisha kukagua hali ya upatikanaji wa vyanzo vya maji na kumkagua mkandarasi anayelaza mabomba eneo la Nyamapinda.
Sanjali na maeneo hayo lakini pia ametembelea ujenzi wa ofisi ya vyombo vya usimamizi wa watumia maji ngazi ya jamii CBWSO, vituo vya ugawaji wa maji kwenye jamii pamoja na zoezi la uchimbaji visima linaloendelea katika kata ya Manda.
Katika ziara hiyo mkuu huyo wa wilaya aliambatana na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa Ndg. Sunday Deogratius, Kamati ya ulinzi na usalama ya Wilaya ya Ludewa, Meneja wa RUWASA Wilaya ya Ludewa Eng. Jeremiah Maduhu pamoja na Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Ludewa Eng. Enock Ngoyinde.