Washiriki wa mafunzo ya wakaguzi wa mbolea wakifuatilia kwa makini mada iliyokuwa ikiwasilishwa na Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Udhibiti Alllan Mariki kuhusu Mamlaka, Majukumu na Maadili ya wakaguzi wa mbolea mkoani Mirogoro.
Maafisa kilimo.kutoka halmashauri mbalimbali nchini wakiwa katika picha ya pamoja na Katibu Tawala Msaidizi Uchumi na Uzalishaji Dkt. Rozalia Rwegasira (wa pili kutoka kulia mstari wa mbele) wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya wakaguzi wa mbolea mkoani Morogoro.
Mwanasheria wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania Bi.Belinda Kyesi akitoa mada kuhusu utekelezaji wa Sheria ya Mbolea Na 9 ya mwaka 2023 na kanuni zake wakati wa mafunzo ya wakaguzi wa mbolea yanayofanyika mkoani Morogoro.
…………………
Wakaguzi wa Mbolea nchini wametakiwa kufanya kazi yao kwa uadilifu na weledi mkubwa ili kuhakikisha kuwa mkulima anapata mbolea yenye ubora unaokubalika.
Wito huo umetolewa na Katibu Tawala Msaidizi Uchumi na Uzalishaji wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Rozalia Rwegasira mkoani Morogoro.
Dkt. Rwegasira amewataka wakaguzi hao, kutenda haki wakati wa utekelezaji wa majukumu yao na kuepuka kabisa vishawishi vyovyote vinavyoweza kuwaingiza katika rushwa na hivyo kuleta madhara katika Taifa kwa ujumla.
Jumla ya maafisa kilimo 20 kutoka halmashauri mbalimbali nchini wanahudhuria mafunzo ya siku tatu kuhusu udhibiti wa mbolea ili kuwajengea uwezo kuwa wakaguzi wa mbolea katika maeneo yao.
Dkt. Rwegasira amesema katika miaka mitano iliyopita Tanzania imekuwa ikitumia tani 300,000 hadi 600, 000 za mbolea kwa mwaka ambayo ni sawa na asilimia 30 hadi 60 ya lengo ambalo ni tani millioni moja.
Ameongeza kuwa serikali ya Awamu ya Sita katika msimu wa 2022/2023 na 2023/2024 imeweka mkakati mahususi wa kuongeza matumizi ya mbolea kwa kutoa ruzuku.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Huduma za Udhibiti, Bwana Allan Mariki amesema Mamlaka imejiwekea lengo la kuwa na wakaguzi wawili kwa kila halmashauri ili kuimarisha ufanisi katika udhibiti wa tasnia ya mbolea nchini.
Mariki amesema mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo na kuwapa mbinu sahihi za udhibiti wa ubora wa mbolea kama zilivyoainishwa kwenye Sheria ya Mbolea Na.9 ya mwaka 2009 na kanuni zake.
Aidha, Bwana Mariki amewataka mawakala na wafanyabiashara wa mbolea nchini kutojihusisha
na vitendo vya kuchezea mfumo wa mbolea za rukuzu kwani hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao wote watakaobainika kufanya hivyo.