Na Sophia Kingimali
Kupitia mkutano wa Mabadiliko ya tabia nchi (Cop28) Kampuni na Taasisi 56 zimeonesha nia ya kuwekeza nchini kwa kushirikiana na sekta binafsi
Hayo ameyasema leo desemba 18,2023 jijini Dar es salaam Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Dkt Suleman Jaffo, wakati akitoa taarifa kuhusu ushiriki wa Tanzania katika Mkutano wa Kimataifa wa Mabadiliko ya tabia nchi (Cop28).
Amesema Kupitia Mkutano wa 28 Tanzania itanufaika zaidi na fedha za miradi, teknolojia, utaalam na Programu mbalimbali za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ikiwemo Programu ya Afrika ya Nishati Safi ya Kupikia; programu ya Afya na mabadiliko ya tabianchi; na utekelezaji wa mikakati ya kuimarisha uhimili katika katika sekta ya maji, misitu na Bahari.
“Wafanya biashara na wawekezaji wa Tanzania walikutana na wawekezaji kutoka nje ya nchi na kujadiliana kuhusu fursa za uwekezaji kwenye eneo la mabadiliko ya tabianchi ambapo jumla ya taasisi na kampuni zaidi ya 56 zimeonesha nia ya kuwekeza nchini kwa kushirikiana na sekta binafsi nchini,”amesema.
Dkt Jaffo amesema Tanzania inapoteza asilimia 2 hadi 3 ya pato la taifa kutokana na mabadiliko ya tabia nchi.
Amesema Tanzania imeshiriki mikutano ya pembezoni ya ngazi ya juu iliyohusu uzinduzi wa Mpango wa kukuza matumizi na nishati safi na nafuu ya kupikia kwa wanawake barani Afrika ulioshirikisha wadau ana kwa ana 150.
“Pia kulikuwa na mkutano wa ngazi ya juu kuhusu fursa za uwekezaji kwenye sekta ya kilimo kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi , mkutano wa kuongeza kasi ya kupambana na mabadiliko ya tabia nchi katika sekta ya kilimo kwa kushughulikia hasara.
Amesema masuala yaliyojadiliwa katika Mkutano huo ni mikakati ya kukusanya Dola za Marekani bil 1.8 kwa ajili ya kuchimba visima 65,000 ambapo kila kisima kimoja kitahudumia wakulima wenye mashamba ya ukubwa wa hekta 2.5.
Amesema programu hiyo itasaidia uhimilivu wa mabadiliko ya tabianchi katika sekta ya Kilimo na itapunguza uharibifu wa mazingira.
Dkt Jaffo amesema katika Mkutano huo sekta binafsi na Asasi za Kiraia (AZAKI) 340 zilishiriki ipasavyo katika mkutano wa COP28 ikiwemo banki ya Kilimo ya Taifa ambazo zilikuwa sehemu kubwa ya wajumbe wa Tanzania walioshiriki katika mkutano huo.
Amefafanua kuwa katika mkutano huo nchi wanachama wa Mkataba wa Kimataifa wa mabadiliko ya tabia nchi zilikuwa na makubaliano 11 ambayo lengo la pamoja la kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi.
Pia uendeshaji wa Mfuko wa kukabiliana na upotevu na uharibifu utokanao na mabadiliko ya tabianchi pamoja na uundwaji wa Bodi ya ushauri ya Mfuko huo.
“Katika Mfuko huu wanachama wamekubaliana kuwa Benki ya Dunia itausimamia Mfuko husika kwa kipindi cha miaka 5 na Sekretarieti ya Umoja wa Mataifa inayoshughulikia Majanga (United Nations Office Disaster Risk Reduction- UNDRR) itakuwa Sekretarieti ya Bodi ya Ushauri, Jumla ya kiasi cha takriban USD Milioni 792 zimeahidiwa kutolewa kwa ajili Mfuko huo,”amesema.
Mkutano huo uliofanyika Dubai, Falme za Kiarabu kuanzia Novemba 30 hadi Desemba 12, 2023 wenye lengo la kupitia taarifa, kufanya kutatmini, majadiliano na maamuzi kuhusu hatua zilizochukuliwa nan chi wanachama katika kufikia malengo ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu mabadiliko ya Tabia nchi.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira.