Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb.) ameainisha mafanikio yaliyopatikana kwa Taifa kutokana na utekelezaji wa Sera ya Mambo ya Nje yenye msisitizo katika Diplomasia ya Uchumi kuwa ni pamoja na kuimarika kwa ushirikiano baina ya Tanzania na nchi nyingine, kukua kwa biashara, uwekezaji na utalii na kuongezeka kwa ushawishi na sauti ya Tanzania katika majukwaa ya kikanda na kimataifa.
Mhe. Makamba ameanisha mafanikio hayo kwenye mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika jijini Dar es Salaam tarehe 17 Desemba 2023 wakati akitoa Tathmini ya Mafanikio ya Wizara katika Kueneza, Kukuza na Kupanua Diplomasia ya Tanzania Kimataifa kwa mwaka 2023 pamoja na kutoa Mwelekeo na Matarajio ya Wizara kwa Mwaka 2024.
Mhe. Makamba amesema kuwa, Diplomasia ya Tanzania chini ya uongozi imara wa Mwanadiplomasia namba moja, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuimarika katika nyanja mbalimbali ambapo kupitia uratibu wa Wizara na kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, Tanzania katika kipindi cha mwaka 2023 imefanikiwa kuimarisha uhusiano ya uwili, kukuza biashara na uwekezaji, kuongeza ushawishi wa Tanzania katika masuala mtambuka yanayohitaji ushirikiano wa kimataifa, kutafuta fedha kwa ajili ya kugharamia miradi ya kimkakati na kuongezeka kwa watalii.
Akifafanua kuhusu kuimarika kwa ushirikiano wa uwili kati ya Tanzania na nchi mbalimbali duniani na mashirika ya kimataifa, Mhe. Makamba amesema kupitia ziara mbalimbali zilizofanywa na Mhe. Rais Dkt. Samia, Viongozi Wakuu Serikalini na zile zilizofanywa na Marais na Wakuu wa Mashirika kutoka nje ya nchi hapa nchini zimeiwezesha Tanzania kunufaika kiuchumi kwa kuimarika zaidi kwa ushirikiano na nchi hizo pamoja na mashirika ya kikanda na kimataifa.
Kadhalika amesema kuimarika kwa ushirikiano huo kumeiwezesha Tanzania katika mwaka 2023 kuwa mwenyeji wa mikutano mikubwa ya kikanda na kimataifa ukiwemo Mkutano wa Kimataifa kuhusu Mifumo ya Uzalishaji wa Chakula na Mkutano wa Kimataifa kuhusu masuala ya Rasilimali Watu.
Pia amesema Wizara imefanikiwa kuratibu Mikutano ya Tume ya Pamoja kati ya Tanzania na nchi mbalimbali zikiwemo Algeria, Comoro, Finland na Indonesia. Kupitia mikutano hiyo, Tanzania ilifanikiwa kujadili masuala mbalimbali ya kuimarisha ushirikiano katika sekta mbalimbali.
Kuhusu kukua kwa biashara na uwekezaji nchini, Mhe. Makamba amesema takwimu zinaonesha kwa kiasi kikubwa kazi imefanyika ambapo Mhe. Rais Dkt. Samia ameongoza ushiriki wa Tanzania kwenye makongamano mbalimbali ya biashara na uwekezaji ikiwemo Kongamano la Biashara kati ya Tanzania na India, Kongamano la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Zambia pamoja na kuelekeza kufanyika kwa makongamano mbalimbali likiwemo lile la Tanzania na Uholanzi na Tanzania na Ufaransa yaliyomshirikisha Mhe. Waziri Makamba.
“Kwenye kukuza biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na nchini mbalimbali, takwimu zinaonesha kazi imefanyika kwa umahiri mkubwa. Mhe. Rais ameongoza kazi hii kama mwanadiplomasia namba moja na kushiriki kwenye makongamano ya biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na India, Tanzania na Zambia lakini pia ameelekeza kufanyika kwa makongamano mengine ambayo tumeshiriki baadhi yetu sisi, Tanzania na Uholanzi, Tanzania na Ufaransa na Tanzania na Ungereza” amesisitiza Mhe. Makamba.
Mhe. Makamba pia amesema kuwa, Tanzania imefanikiwa kupanua masoko ya bidhaa zake mbalimbali duniani ikiwemo kupatikana kwa soko la Mbaazi na Korosho nchini India na Vietnam na Mkonge nchini China na Brazil na Maparachichi nchini China na nchi za Ulaya. Amesema kupanuka kwa masoko ya bidhaa hizo kutaongeza uzalishaji, ajira na kipato na hatimaye kuchangia maendeleo ya Taifa.
Kuhusu utafutaji fedha za kugharamia miradi ya maendeleo hapa nchini, Mhe. Waziri Makamba amesema jukumu hili limetekelezwa kikamilifu ambapo kupitia mawasiliano yaliyofanyika kati ya Tanzania na Mashirika mbalimbali ya kimataifa yanayotoa misaada na mikopo ikiwemo Benki ya Maendeleo ya Afrika, Mfuko wa Kuwait, Shirika la Fedha Duniani na mengine yamefanikisha upatikanaji wa fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa Reli ya Kisasa.
Waziri Makamba amesema kutokana na kazi za nzuri inayofanywa na Mwanadiplomasia namba moja, Mhe. Rais Dkt. Samia sauti na ushawishi wa Tanzania katika masuala mtambuka imeendelea kusikika huku akitoa mfano wa Mkutano wa 28 wa Kimataifa wa Mambadiliko ya Tabianchi uliofanyika Umoja wa Falme za Kiarabu mwezi Desemba 2023 ambapo Mhe. Rais Dkt. Samia alifanikisha kufanyika kwa mkutano wa pembezoni kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia ili kuepuka ukataji wa miti hovyo.
Kadhalika amesema kutokana na Diplomasia ya Tanzania kuimarika, Mhe. Rais Dkt. Samia ameteuliwa kwenye nafasi mbalimbali ikiwemo kuwa Championi wa Dunia kwenye masuala ya usawa wa kijinsia.
Pia Mhe. Makamba amesema kuwa, Tanzania kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imefanikiwa kuimarisha ujirani mwema na nchi mbalimbali, jumuiya za kikanda na kudumisha amani na usalama katika kanda.
“Tanzania ni mwenyekiti ajaye wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kupitia nafasi hii Tanzania itaendelea kutoa mchango wake katika kuimarisha amani na usalama katika kanda hii” amesema Mhe. Makamba.
Akielezea mwelekeo na matarajio ya Wizara kwa mwaka 2024, Mhe. Makamba amesema Wizara itaendelea kutekeleza Sera ya Mambo ya Nje inayosisitiza katika Diplomasia ya Uchumi; Kukamilisha uandaaji wa Sera Mpya ya Mambo ya Nje ili iendane na mazingira ya sasa ya dunia; kukamilisha uratibu wa Hadhi Maalum kwa Diaspora; Kupanua uwakilishi wa Tanzania kwa kufungua Balozi mpya; Kuwa mwenyekiti wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC kwa kipindi cha mwaka mmoja; Kuratibu mikutano ya Tume za Pamoja za Ushirikiano na nchi mbalimbali; Kuandaa makongamano ya biashara kati ya Tanzania na nchi mbalimbali; Kuratibu na kuwa mwenyeji wa mikutano mbalimbali ya kikanda na kimataifa na kuratibu ziara za Mhe. Rais na Viongozi wengine wakuu wa Serikali.