…………………………. Na Muhidin Amri,
Lindi
BAADHI ya wananchi wa kijiji cha Mputwa kata ya Kiwawa wilaya ya Lindi mkoani Lindi,wameishukuru serikali kwa kukamilisha mradi wa maji Mputwa uliojengwa kwa gharama ya Sh.milioni 490.
Walisema tangu Uhuru hawajawahi kupata maji ya bomba,badala yake walitumia maji yanayopatikana kwenye mito na maporomoko ambako kuna wanyama wakali kama fisi na Tembo na maji yake hayakuwa safi na salama.
Said Mandiki(67) alisema,serikali kupitia Ruwasa imewatendea haki wananchi wa kijiji hicho kwa kutekeleza mradi huo na kuhaidi kuutunza ili uweze kunufaisha vizazi vya sasa na baadaye.
Mohamed Issa,amewapongeza wataalam kutoka wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa)wilaya na mkoa wa Lindi kukamilisha mradi huo uliomaliza mateso ya kutembea umbali mrefu na kutumia muda mwingi kwenda kutafuta maji kwenye vyanzo vya asili.
Zuhura Said alisema,awali walikuwa wanatoka nyumbani kati ya saa 9 na 10 usiku kwenda kutafuta maji na kurudi saa 1 asubuhi,hali iliyosababisha baadhi ya wanawake wa kijiji hicho kujikuta wakiingia kwenye migogoro ya ndoa zao mara kwa mara.
Zuhuru,amemshukuru Rais Samia kutoa fedha zilizotumika kutekeleza mradi huo na hivyo kusaidia kuokoa ndoa za wanawake wa kijiji hicho ambao kwa muda mrefu hawakuwa na furaha kwenye maisha yao.
Meneja wa wakala wa maji safi na usafi wa mazingira Ruwasa wilaya ya Lindi Idd Pazi alisema,utekelezaji wa mradi wa maji Mputwa umelenga kuondoa kabisa changamoto ya ukosefu wa maji katika kijiji hicho na vitongoji vya jirani.
Pazi alisema,mradi huo umetekelezwa kwa gharama ya Sh.milioni 492,678,506.00 na utekelezaji wake umefikia asilimia 97 na kwa sasa umeanza kutoa huduma ya maji kwa wananchi wa kijiji hicho tangu mwezi Julai mwaka huu.
Alitaja kazi zilizotekelezwa ni ujenzi wa banio(chanzo cha maji)kujenga tenki dogo,nyumba ya kuhifadhi mitambo ya kusukuma maji na mlinzi na kujenga tenki la lita 50,000 kwenye mnara wa mita 6.
Pazi alitaja kazi nyingine zilizotekelezwa ni ujenzi wa mtandao wa bomba la kugawa maji wenye urefu wa kilomita 3.4,ujenzi wa vituo vya kuchotea maji 4 na kujenga ofisi ya chombo cha watumia maji ngazi ya jamii(CBWSO) na mkandarasi anaendelea na kazi za umaliziaji wa ujenzi wa mradi huo.