VICTOR MASANGU,KIBAHA
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe.Abdallah Ulega ametoa rai kwa wafugaji nchini kuilisha mifugo yao nyasi zilizoboreshwa aina ya Juncao ili kuongeza uzalishaji wa Maziwa na Mazao mengine yatokanayo na wanyama kuifikia tija kwenye sekta ya ufugaji.
Mhe.Ulega ameyasema hayo alipotembelea Shamba la malisho Vikuge,Wilaya ya Kibaha, Mkoa wa Pwani alipofanya ziara rasmi ya Kikazi ambapo alitembelea pia Kiwanda cha Kuchakata nyama cha Tanchoice pamoja na Kiwanda cha kutengeneza Chanjo za Wanyama cha Hester Biosciences African Limited kilichopo eneo la Viwanda TAMCO,Halmashauri ya Mji Kibaha.
Meneja wa Shamba la Vikuge Reuben Ngailo,amesema kuwa Juncao ni aina ya nyasi lishe iliyotokana na Maboresho ya majani ya tembo/Napier (Pennisetum spp) yenye viini lishe vingi Mathalani Protoni ghafi 16%-18% ukilinganisha nyasi zingine ambapo uzalishaji wake hufikia Tani 170 kwa ekari moja na huvunwa kati ya miezi 2-3 kwa Matumizi ya chakula na miezi 6-7 kwa ajili ya Matumizi ya Mbegu.
Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Dkt.Samia Suluhu Hassan,Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilitoa jukumu kwa Shamba la malisho Vikuge kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuendeleza jitihada za upatikanaji wa Mbegu za Juncao zitakazowafikia wafugaji wengi ili kuongeza uzalishaji wa Maziwa,Kufuga kwa tija pamoja na kuongeza kipato ngazi ya Jamii na Taifa.
Nyasi zingine zinazopatikana Shamba la malisho Vikuge ni nyasi zilizoboreshwa;Cenhrus ciliaris (buffer grass),Chloris Gayana (Rhodes grass) na Brachiaris Spp.Aidha,Kwa upande wa nyasi asili zipo;Panicum Maximum,Hyperhenia rufa, Heteropogon Conturtus na Cynodon spp
Pamoja na hizo,zipo nyasi za Jamii ya Mikunde kunde kama;Tropical Kudzu,Centrocema spp,Blue pea, Colopogonium spp, Mucuna spp,Canavalia,Ciratro na Marejea.Kwa upande wa Nyasi lishe kando ya Juncao zipo pia;Napier,Sugar Maize,Guatemala na Maize.Aidha,kwa upande wa Miti lishe ni;Sesbania spp,Leucaena spp,Acacia spp na Grilicidia spp.
Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Mhe.Nickson Simon John amesema uwingi wa aina za nyasi za Kisasa kwenye Shamba la Malisho Vikuge ni fursa kwa wananchi wa Tanzania hususan wa Kibaha kufuga Kisayansi ili kupata matokeo chanya.