Na Sophia Kingimali,Dar es salaam
Jamii imetakiwa kujiepusha na tabia bwete na kuhakikisha wanafanya shughuli za kushughulisha mwili kwa kazi tofauti kila baada ya dakika 60 kama vile kusimama,kutembea,kukimbia au jambo lolote la kushughulisha mwili kujiepusha na magonjwa yasiyo ya kuambukiza.
Wito huo umetolewa Decemba 14, 2023 katika semina kwa wanahabari iliyoandaliwa na Chama Cha Wanasheria Wanawake (TAWLA) kuhusu uchechemuzi wa sheria ya mtindo wa maisha na magonjwa yasiyo ya kuambukiza ili kusaidia jamii kupitia sheria kuzingatia kanuni za afya zinazosaidia kuepukana na magonjwa hayo ambayo yanarudisha nyuma uchumi wa Taifa na wa mtu mmoja mmoja.
Akizungumza katika semina hiyo Dkt. Waziri Ndonde amesema namna ya kujenga mwili ni lazima kufanya kazi za kushughulisha mwili kama kutembea,kukimbia,kufanyakazi za nyumbani,kutumia baiskeli pamoja na kushiriki kwenye michezo mbalimbali.
“Kama unafanya mazoezi peke yake lakini haushughulishi mwili baada ya mazoezi uwezi kupata matokeo unayoyataka na hivi ndio utasikia mtu anasema mimi naenda (Gym) kila siku lakini sipungui” amesema Dkt Ndonde.
Aidha Dkt Ndonde amebainisha kuwa katika kanuni bora za afya ya mwili na akili ni lazima kufanya mazoezi ya kuhushughulisha mwili ambapo watoto na vijana kati ya miaka 5-17 wanatakiwa kutumia Dakika 60 katika michezo na mambo ya kushughulisha mwili kila siku huku watu wazima kati ya miaka 18-64 na pamoja na watu wenye magonjwa sugu wanashauriwa kutumia Dakika 150 kwa wiki ndani ya siku tano wafanye mazoezi ya uzito wa kati na siku mbili wanatakiwa kufanya mazoezi ya misuri ndani ya dakika 30.
Akizungumzia walemavu Dkt. Ndonde amesema ulemamu wao wanapaswa kufanya mazoezi kwa al dakika 300 kwa wiki
Pia amesisitiza kuwa wanawake wajawazito na waliojifungua wanapaswa kufanya mazoezi kwa dakika 150 kwa wiki ambapo mazoezi hayo yatasaidia kuimarisha misuli.
“Tafiti zinaonyesha kujifungua na kunyonyesha sio sababu ya kunenepa, watu wengi wanakula kupitiliza na kuacha mazoezi pindi wanapojifungua”Amesema Dkt. Ndonde na kuongeza kuwa
“Kufanya mazoezi kunaufanya ubongo wako unafanyakazi vizuri pia kuna ongeza uwezo wa moyo kufanyakazi vizuri”.
Akizungumza katika semina hiyo Dkt. Fredrick Mashil kutoka Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) amesema magonjwa yanazuilika lakini matibabu yake pindi utakapoyapata ni gharama sana.
“Vitu vikubwa vinasababisha mangonjwa yasiyo ya kuambukiza ni pamoja na (Diet) kufanya mazoezi kupitiliza na mtindo wa maisha,” amesema Dk. Mashil.
Amesema kama nchi haina sheria na sera yeyote ambayo inazuia kula vyakula ambavyo vinaathiri afya ya walaji ndio maana bado watu wanatumia vyakula hivyo.
“Nimefanya utafiti wa mafuta ya kula yanatumika na watu wengi mafuta ya kula yanayotokana na mimea ni mazuri kutumika kiafya lakini mafuta ya kula yatokanayo na wanyama sio mazuri kiafya hivyo niwashauri watu watumie mafuta ya kula yanatokana na mimea “ameeleza.
Ameongeza kuwa zaidi ya vifo 25000 vinapungua kwa kuondoa bidhaa zinazoathiri afya ya walaji hivyo watu wanaishi zaidi ya miaka 25 ijayo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Vijana wenye Kisukari Tanzania ( TDYA), George Kwayu ameiomba serikali kuangalia namna bora ya kuwasaidia wagonjwa wa kisukari kutokana na matibabu yake kuwa gharama hali inayopelekea vijana wengi kupoteza maisha kwa kushindwa kumudu gharama za matibabu.
Pia wamewataka wagonjwa wa ugonjwa huo kuikubali hali hiyo huku ambao sio wagonjwa kujikinga na kuzingatia kanuni za afya na kufanya mazoezi ili kujiepusha na tabia bwete
“Mtu yeyote anaweza kuwa na ugonjwa wa kisukari ni jambo la kujikubali pindi unapogundulika lakini pia kujikinga usikupate kwani magonjwa yasiyo yakuambukiza yamekua na athari kubwa lakini yanazuilika hivyo ni vyema kuyazuia Maana ukiyapata yanaathari kubwa kwa jamii lakini pia nchi”amesema.
Aidha Kwayu amewashauri wagonjwa wa kisukari kwamba matibabu yanapatikana hospitali na kuna watalaamu wazuri hivyo ni vyema vijana kupima afya zao ili waweze kujitambua lakini pia kuchukua tahadhari ya magonjwa yasiyoambukiza.