Na Sophia Kingimali,Dar es salaam.
Wadau wa kodi nchini wameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kusikia kilio chao na kuanzisha Taasisi ya Usuluhishi wa Malalamiko na Taarifa za Kodi (TOST) ambapo taasisi imewahakikishia wadau hao kwamba malalamiko yatashughulikiwa kama yalivyowasilishwa huku ikisisitiza ukweli katika kutatua tatizo.
Hayo yamejiri jijini Dar es Salaam, desemba 15,2023 katika kikao cha TOST na wadau wa kodi kilicholenga kuitambulisha taasisi hiyo huru iliyoko chini ya Wizara ya Fedha na kueleza dhumuni lake.
Wadau hao kwa nyakati tofauti wakiwasilisha hoja, wameishukuru serikali chini ya Rais Dk Samia kwa kuanzisha chombo hicho, huku wakitoa ushauri na kuhoji masuala mbalimbali.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania (JWT), Khamis Livembe ameishukuru serikali kwa kuunda chombo hicho na kusema kitakapotumika vyema kitasaidia kuondoa migogoro ya kodi.
Kwa upande wake Katibu wa Jumuiya ya Wafanyabiashara, Mkoa wa Tanga, Ismail Masoud amesema chombo hicho walikuwa wanakililia muda mrefu, hivyo kuundwa kwake kutaisaidia serikali na wafanyabiashara kubaini tatizo la kodi.
Katibu Mtendaji wa Chama Cha Mawakala wa Forodha Tanzania, Elitunu Mallamia, amesema kuanzishwa kwa TOST ni jambo jema kwa kuwa ni sikio la serikali kuhusu malalamiko ya walipa kodi na inawaasa walipa kodi kulipa kwa hiari.
Ameiomba TOST iishauri serikali na taasisi zake za kodi kuhusu viwango vya kodi na uboreshwaji wa tozo.
Kwa upande wake Msuluhishi wa Malalamiko na Taarifa za Kodi (TOST) Robert Manyama amesema lengo la mkutano huo ni kuitambulisha taasisi hiyo huru kwa wadau, kueleza malengo yake, falsafa za usuluhishi na kutoa wito kwa Watanzania kuitumia taasisi hiyo ambapo gharama za usuluhishi zinalipwa na serikali.
Amesema taasisi ipo huru na dhamira ya kuanzishwa kwake ni kutoa huduma bora katika kushughulikia malalamiko ya kodi kwa usawa na kwa ufanisi.
Manyama amesema kwa mujibu wa sheria wanatakiwa kushughulika lalamiko ndani ya siku 30 na siku 14 kupeleka ripoti kwa waziri na pendekezo hususan pale panapotokea ubishi kati ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na mlipa kodi.
Amesema wanatumia mbinu za usuluhishi zinazoacha uhusiano mwema kati ya mlalamikaji na mlalamikiwa na wanashirikiana na taasisi zinazofanya tafiti katika maeneo ambayo wameona yana tatizo.
“Pande zote zinasimama katika usawa kila mmoja apatiwe haki ya kusikilizwa na kuheshimiana wakati wa kushughulikia lalamiko,” amesema.