Na Issa Mwadangala
Wazazi na walezi wilayani Songwe wametakiwa kuwa karibu na watoto wao kama wanavyokuwa karibu na simu zao ili kujua ukatili wanaofanyiwa wakiwa nyumbani, njiani, mtaani au shuleni ili kubaini na kudhibiti ukatili huo mapema kwa kutoa taarifa Polisi kwani kufanya hivyo kutapunguza vitendo vya ukatili dhidi ya watoto.
Akizungumza wakati alipohudhuria ibada ya Jumamosi katika kanisa la Waadventista la Wasabato Desemba 16, 2023 lililopo Mkwajuni, Kamanda wa Polisi mkoani Songwe Kamishna Msaidizi wa Polisi ACP Theopista Mallya, alisema unakuta mzazi ajui mtoto wake ameshindaje, yupo wapi, anacheza na nani na wanacheza michezo gani yeye kutwa na miangaiko yake bila kumuangalia mtoto wake hili linapelekea mtoto kufanyiwa ukatili inapaswa mzazi/mlezi kufuatilia makuzi ya mtoto wako ili kumuepusha kufanyiwa vitendo vya ukatili na unyanyasaji.
“Mzazi anaona bora zaidi kufunga biashara yake na kwenda nyumbani kufuata simu aliyoisahau kuliko kumuangalia mtoto wake kama simu yake, sasa basi unapaswa unavyoilinda na kuiangalia simu yako hivyohivyo unatakiwa kumuangalia mtoto wako ili kuwa na kizazi bora na chenye maadili” alisema Kamanda Mallya.
Sambamba na hayo Kamanda Mallya alikabidhiwa vitabu vya Injili ili aendelee kuhubiri na kukemea uovu, hili limefanyika katika kanisa hilo baada ya kutoa Elimu juu ya utoaji taarifa za ukatili wa kijinsia na unyanyasaji dhidi ya watoto.
Nae Mchungaji wa kanisani hilo Moses Kihinga aliwataka waamini hao kuonesha mabadiliko kwenye jamii kwa kutenda matendo yaliyo mema ikiwa ni pamoja na kuwapa malezi bora watoto wao ili kuwa na kizazi kilicho bora na chenye maadili mema katika ujenzi wa taifa letu.