Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na viongozi pamoja na wageni mbalimbali waliohudhuria Maadhimisho ya miaka 50 ya Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA) yaliofanyika katika Ofisi za Baraza hilo Jijini Dar es Salaam Desemba 16, 2023.
Viongozi pamoja na wageni mbalimbali wakiwa kwenye maadhimisho ya miaka 50 ya Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA) katika Ofisi za Baraza hilo Jijini Dar es Salaam tarehe 16 Desemba, 2023.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akipokea kitabu cha miaka 50 ya Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA) kutoka kwa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda wakati wa Maadhimisho ya miaka 50 ya Baraza hilo katika Ofisi za Baraza hilo Jijini Dar es Salaam tarehe 16 Desemba, 2023.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwasili katika viwanja vya Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA) kwa ajili ya kushiriki kwenye maadhimisho ya miaka 50 ya Baraza hilo Jijini Dar es Salaam tarehe 16 Desemba 2023.
………………………
Na Sophia Kingimali
RAIS Dk.Samia Suluhu Hassan ameiagiza Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia kushirikiana na Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kufunga mtandao katika vijiji vyenye umeme kuwawezesha wanafunzi waliopo pembezoni mwa miji kujifunza na kufanya mitihani ya masomo ya sayansi kwa kutumia teknolojia.
Kauli hiyo ameitoa jijini Dar es Salaam leo Desemba 16,2023 katika kilele cha maadhimisho ya miaka 50 ya Baraza la Mitihani Tanzania(NECTA) na amesema serikali itaendelea kupeleka umeme katika maeneo mbalimbali hasa vijijini kuwawezesha wanafunzi wa sayansi wasiokuwa na walimu wa kutosha kusoma kwa kutumia teknolojia.
“Kutokana na watahiniwa wote kutahiniwa sawa bila kujali mazingira na changamoto yoyote, serikali itaendelea kupeleka umeme katika maeneo mbalimbali hasa vijijini kuwawezesha wanafunzi hasa wa sayansi ambao hawana walimu wa kutosha ,wasome kwa kutumia mfumo wa kimtandao unaotekelezwa na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote(UCSAF),” amesema.
Amesema mfumo huo umekuwa na matokeo chanya kutokana na wanafunzi wanaoutumia kufanya vizuri katika masomo yao.
Vilevile Rais Dk. Samia amesema mfumo huo umesaidia kupunguza gharama ya kununua vifaa vya maabara kwa wizara kwani mwanafunzi anaviona katika mtandao na anaweza kufanya mtihani au kusoma kwa mtandao.
Amesema serikali imefanya uwekezaji mkubwa katika Tehama ambao umeimarisha utendaji wa Baraza hususani katika matumizi ya teknoliojia katika usajili wa watahiniwa, uchapaji, usahihishaji wa mitihani na uchakataji wa matokeo.
Kwa upande wake Spika wa Bunge, Dk.Tulia Ackson amelipongeza baraza hilo kwa kutumiza miaka 50, kwani ni muda muafaka wa kutafakari lilipotoka, lilipo na linapokwenda.
Amesema bunge litaendelea kutoa ushirikiano kwa kulisimamia na kulishauri baraza hilo kutimiza malengo yaliyokusudiwa.
Kwa upande wake,Waziri wa Habari,Mawasiliano na Teknolojia ya Habari,Nape Nnauye amesema tayari wizara imeshaanza kufanya tathmini ya idadi ya shule zilizopo katika kila halmashauri.
Pia, amesema wamefanya tathmini ya gharama zitakazohitajika kufunga mifumo hiyo ya Tehama kuwawezesha wanafunzi wa sayansi waliopo pembezoni mwa miji kujifunza masomo ya sayansi kwa shule zinapopatikana maabara.
Naye Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda amesema ndani ya miaka 50 ya NECTA, wamefanikiwa kudhibiti wizi wa mitihani ukilinganisha na nchi nyingine.
“Kwa yoyote atakayejaribu kuiba mitihani hasa kwa mfumo wa taasisi tutamchukulia hatua kali kwa sababu Baraza la Mitihani liko macho kila kukicha,” amesema.
Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa NECTA, Dkt. Said Mohomed alitoa pole kwa waathirika wa mafuriko wilayani Hanang, mkoani Manyara na kuahidi kuwapa vyeti mbadala waliopoteza vyeti vyao katika maafa hayo.
Hata hivyo amesema Baraza hilo likijikita kuwekeza zaidi katika Tehama kwa kutoa elimu kwa njia ya mtandaoni.