Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis akizungumza na wananchi mara baada ya kukabidhi boti ya uvuvi kwa kikundi kilichopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Mradi wa Hifadhi ya Ardhi ya Bonde la Ziwa Nyasa Halmashauri ya Nyasa mkoani Ruvuma.
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis akikagua boti iliyotolewa kupitia Mradi wa Hifadhi ya Ardhi ya Bonde la Ziwa Nyasa unaoratibiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais na kutekelezwa katika Halmashauri ya Nyasa mkoani Ruvuma.
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis akiwa amepanda boti ya uvuvi iliyotolewa kupitia Mradi wa Hifadhi ya Ardhi ya Bonde la Ziwa Nyasa unaoratibiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais na kutekelezwa katika Halmashauri ya Nyasa mkoani Ruvuma. Kushoto ni Mbunge wa Jimbo la Nyasa Mhandisi Mhe. Stella Manyanya.
……………………………
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis ametoa wito kwa wananchi kuitunza miradi ili ifikie malengo katika hifadhi ya mazingira.
Ametoa wito huo wakati alipofanya ziara ya kikazi ya kukagua na kufuatilia utekelezaji wa Mradi wa Hifadhi ya Ardhi ya Bonde la Ziwa Nyasa mkoani Ruvuma.
Akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Ndumbi mara baada ya kukabidhi boti mbili za uvuvi na injini zake kwa kikundi cha Kivukoni Vikoba kikundi kilichopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa, Mhe. Khamis amesema kuwa mazingira ya majini ni muhimu kutunzwa ili kuwe na tija katika uvuvi.
Amewaasa wavuvi kufanya uvuvi endelevu usioharibu mazingira ya maji na viumbe vyote vilivyomo huku akiwataka wananchi kuacha kutupa taka au vitu ovyo ili visje vikaharibu mazingira na kudhuru viumbe wa majini.
Akiendelea kuzungumza na wavuvi na wananchi, Naibu Waziri Khamis amewahimiza wananchi kuhakikisha kuwa wanatunza vyanzo vya maji visikauke ili vinufaishe vizazi vilivyopo na vijavyo.
Amewapongeza wanakikundi hao kwa kuutunza mradi na kutumia sehemu ya faida waliyopata na kununua boti nyingime mbili na injini zake hivyo kuongeza tija katika shughuli za uvuvi.
Aidha, Naibu Waziri amesema baadhi ya mito na vyanzo vingine vya maji katika maeneo mbalimbali vimekauka kutokana na watu kufanya shughuli za uharibifu wa mazingira hivyo ametoa rai kutunza mazingira.
“Nimepita mikoa mbalimbali nimeona vyanzo vya maji vinakauka lakini kwa hapa katika Wilaya hii ya Nyasa sehemu nyingi nilizopita nimeona maji yanatiririka inaonesha namna gani mnatunza vyanzo vya maji, sasa nawasihi muendelee kuvitunza,“ amesisitiza.
Hali kadhalika Naibu Waziri amewasihi wananchi kuunga mkono juhudi za Serikali inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ambayo inawaletea wananchi maendeleo.
“Ndugu zangu Rais wetu Mama Samia anafanya kazi kubwa sana na tunashuhudia Serikali yake inaendelea kuhakikisha inawapatia wananchi huduma zikiwemo za maji kupitia miradi mbalimbali,“ amesema Naibu Waziri Khamis.
Kwa upande wak Mbunge wa Jimbo la Nyasa Mhandisi Mhe. Stella Manyanya ameishukuru Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kuratibu na kutekeleza Mradi wa Hifadhi ya Ardhi ya Bonde la Ziwa Nyasa.
Amesema mradi huo umesaidia wananchi waliokuwa wanafanya shughuli zinazoharibu mazingira kuachana nazo na kuanza kuhifadhi mazingira hususan katika Bonde la Ziwa Nyasa.
Mhe. Manyanya amesema kupitia boti hizo zilizokabidhiwa kupitia mradi huo zinawasaidia wavuvi kuboresha shughuli za uvuvi ambapo hivi sasa wameanza kuvua samaki kwa wingi.