.,,,…………..
Na Sixmund Begashe
Serikali chini ya Mhe Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imefanya maamuzi muhimu ya kuimarisha uhifadhi na kukuza utalii Kusini mwa Tanzania kupitia mradi wa REGROW, hivyo watekelezaji wa mradi watakiwa kuhakikisha malengo ya mradi yanafikiwa kwa ufanisi ili nia njema ya Serikali iweze kuwainua wananchi kiuchumi.
Akifungua kikao cha kamati ya uongozi wa Mradi wa Kuboresha Usimamizi wa Maliasili na Kukuza Utalii Kusini mwa Tanzania (REGROW), Mkoani Morogoro, Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii Dkt. Hassan Abbasi amesema hadi sasa sekta ya utalii inaongoza kwa kuingiza fedha za kigeni nchini, na hadi sasa Dola za Kimarekani zaidi ya bilioni tatu zimesha patikana kupitia Utalii hivyo mradi wa REGROW utakapo ifungua Kusini, nchi itaongeza mapato zaidi.
Aidha Dkt. Abbasi ameongeza kuwa, kwa mujibu wa Shirika la Utalii Duniani , Tanzania ni Moja ya nchi zinazokuwa kwa kasi kwa ongezeko la watalii kutoka mataifa nje, kwa nchi za Afrika ni namba mbili kwa ongezeko la asilimia 19, ikilinganishwa na kipindi cha UVIKO 19, na ni nafasi ya 12 Duniani. Hivyo kupitia mradi wa REGROW Tanzania inatarajiwa kushika nafasi ya juu zaidi.
Dkt. Abbasi amesisitiza kuwa serikali inawekeza kwenye sekta ya utalii ikilenga kutengeneza ajira zaidi kwa watanzania na kuinua uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla. Hadi sasa wanachi wameshaanza kunufaika na mradi huo kiuchumi huku uhifadhi wa Maliasili unaendelea kuimarika.
Kikao hicho kimeudhuriwa na wajumbe kutoka Wizara mbalimbali na Taasisi zinazotekeleza mradi wa REGROW pamoja na wasimamizi wa mradi huo kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii.