Na Issa Mwadangala
Viongozi wa dini wamekumbushwa kuwa suala la kukemea uhalifu ni jukumu la kila mmoja ikiwemo kutoa taarifa za vitendo vya uhalifu na vitendo vya ukatili wa kijinsia na Unyanyasaji dhidi ya Watoto vinavyofanyika kwenye maeneo yao.
Kauli hiyo imetolewa na Kamanda wa Polisi mkoa wa Songwe, Kamishna Msaidizi wa Polisi ACP Theopista Mallya alipohudhulia kwenye swalat Ijumaa Desemba 15, 2023 katika Msikiti wa Jamalil Islamiyya uliopo Mkwajuni mkoani Songwe.
Kamanda Mallya alitumia fursa hiyo kuwaomba viongozi wa dini ya kiislamu kuendelea kukemea mambo mbalimbali ambayo yanapelekea mmomonyoko wa maadili katika taifa letu ili kuwa na taifa bora na imara.
Alihitimisha kwa kusema katika ziara zake imeonesha kuwa kuna mambo ambayo utatuzi wake unahitaji ngazi nyingine mfano migogoro ya ardhi, kesi kuchukua muda mrefu mahakamani ikiwa ni pamoja na migogoro katika baadhi ya taasisi za kidini ambapo amewahakikishia kuzifikisha katika ngazi husika ili ziweze kupatiwa ufumbu wa haraka.
Kwa upande wa viongozi wa msikiti huo walimpongeza Kamanda wa Polisi mkoa wa Songwe na wameeleza kufurahishwa na ujio wake ndani ya wilaya ya Songwe na waliahidi kuendelea kutoa ushirikiano wa dhati kwa kupeleka elimu hiyo katika maeneo yao.