Na Sophia Kingimali,Dar es salaam
Waziri wa nchi ofisi ya Rais,mipango na uwekezaji Profesa Kitila Mkumbo ametangaza rasmi kuzifuta taasisi za umma nne na kuziunganisha taasisi 16 lengo likiwa kuimarisha utendaji kazi wa mashirika ya umma ili yaweza kuendelea kutoa mchango katika maendeleo ya Taifa.
Akizungumza na waandishi wa habari leo disemba 15,2023 jijini Dar es salaam Profesa Kitila amesema kufuatia hotuba ya Rais Dk.Samia Suluhu Hassan aliyoitoa bungeni April 22,2022 alielekeza kufanya mapitio na uchambuzi wa kina kwa mashirika ya umma ili yaweze kujiendesha kwa faida.
Amesema kwa muktadha huo serikali iliunda timu ya wataalam kwa ajili ya kufanya uchambuzi wa kina kuhusu utendaji wa mashirika hayo kwa lengo la kubainisha changamoto za kiutendaji na kupendekeza hatua za kuchukua katika kuongeza tija ya maendeleo nchini.
“Katika awamu ya kwanza serikali umeridhia na kuelekeza kuunganishwa kwa mashirika na taasisi 16 na kufuta mashirika na taasisi nne”amesema
Taasisi na mashirika yaliunganishwa ni Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) naW akala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA),Benki ya Kilimo Tanzania (TADB) na
Mfuko wa Pembejeo za Kilimo (AGITF)
zinaunganishwa ili kuwa na taasisi moja itakayohusika na mikopo na
ugharamiaji wa maendeleo ya kilimo nchini.
Bodi ya Chai inaunganishwa na Wakala wa Maendeleo ya Wakulima Wadogo wa Chai Tanzania (TSHDA)
zinaunganishwa ili kuwa na bodi moja. (Bodi ya chai).
Bodi ya Nyama inaunganishwa na Bodi ya Maziwa zinaunganishwa ili kuunda
taasisi moja ya kuendeleza na kusimamia mazao ya mifugo yakiwemo ya nyama na maziwa
Kituo cha Zana za Kilimo na Teknolojia Vijijini (CARMARTEC), Taasisi ya Uhandisi na Usanifu Mitambo Tanzania (TEMDO) na Shirika la Kuhudumia
Viwanda Vidogo (SIDO) zinaunganishwa ili kuunda taasisi moja.
Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kinaunganishwa na Mamlaka ya Uzalishaji kwa Mauzo ya Nje (EPZA) ili kuunda taasisi moja itakayoratibu uwekezaji wa sekta binafsi wa ndani na kutoka nje ya nchi.
Taasisi ya Utafiti wa Chai Tanzania (TRIT), Taasisi ya Utafiti wa Tumbaku Tanzania (TORITA) na Taasisi ya Utafiti wa Kahawa (TACRI) zinaunganishwa na kuwa sehemu ya muundo wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI).
Mashirika na Taasisi za Umma zinazofutwa/kuvunjwa ni pamoja na Shirika la Uzalishaji la Jeshi la Polisi (TPFCS),Taasisi ya Chakula na Lishe (TFNC)
Huku Shirika la Elimu Kibaha (KEC) linavunjwa na kuunda Shule ya Sekondari Kibaha ama kwa jina ambalo Mamlaka husika
zitaamua na Chuo Cha Ufundi.
“Kwa uamuzi huu hospitali ya Tumbi Kibaha haitakuwa tena sehemu ya Shirika la Elimu Kibaha bali hospitali ya Mkoa wa Pwani. Msajili wa Hazina ameshaelekezwa kukamilisha taratibu husika za makabidhiano na Wizara ya Afya”ameongeza.
Aidha Bodi ya Pareto inafutwa na shughuli zake zitahamishiwa katika Mamlaka ya Usimamizi wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA).
Aidha Profesa Kitila amewatoa wasisi watumishi wote wa umma walio kwenye taasisi hizo kuwa hakuna mtumishi atakae poteza ajira yake maslahi yao yote yatalindwa na kuzingatiwa kwa kufuata sheria na kanuni za utumishi wa umma.