Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne Mhe. Dkt. Jakaya Kikwete ameupongeza Uongozi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) kwa kuendelea kuzalisha wataalam wenye weledi katika fani mbalimbali za sekta za usafiri na usafiri kulingana kwa kuzingatia mahitaji ya soko.
Akizungumza katika Mahafali ya 39 ya Chuo hicho jijini Dar es Salaam Mhe. Dkt. Jakaya Kikwete amesema pamoja na uzalishaji wa wataalam uongozi wa NIT unatakiwa kuzingatia misingi ya uanzishwaji wake kwa kuzalisha wataalam wengi zaidi kwenye ngazi ya astashada na stahada ili kuweka ulinganifu katika tasnia ya Usafirishaji.
“Vyuo hivi vilianzishwa kimkakati ili kuhakikisha ngazi za wataalam kuanzia ngazi ya chini mpaka ya juu inakwenda sawa sawa hivyo zingatieni misingi hiyo wakati mnaendelea kufanya maboresho mbalimbali ya mitaala’ amesema Mhe. Dkt. Kikwete.
Mhe. Dkt. Kikwete ametumia nafasi hiyo kuipongeza Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuendelea kuwekeza kwenye miundombinu inayokwenda sambamba na uzalishaji wa wataalam ili kuhakikisha kuna mwendelezo katika utekelezaji na uendeshaji wa miradi hiyo.
Aidha, Mhe. Dkt Kikwete ameipongeza NIT kwa kuanzisha kozi za urubani kwani kuanza kwa kozi hizo kutaongeza idadi ya marubani nchini husussani wakati huu ambao Serikali inaendelea na ununuzi ya ndege za masafa marefu na mafupi.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Uchukuzi David Kihenzile amesema Serikali itaendelea kutenga fedha kila mwaka ili kuboresha miunndombinu ya chuo hicho ambapo kwa mwaka huu imenunua ndege mbili za injini moja kwa ajili ya mafunzo katika shule ya Usafiri wa anga chuoni hapo.
Naye Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi la NIT Profesa Ulingeta Mbamba amemuhakikishia mgeni rasmi kuwa baraza hilo litaendelea kusimamia kwa karibu uendeshaji wa chuo hicho ili kuhakikisha wataalam wanaozalishwa wanakidhi mahitaji ya soko katika Nyanja zote za uchukuzi.
Prof. Mbamba ameishukuru Serikali kwa kutoa fedha za utekelezaji wa miradi mbalimbali ya chuo kwani kupitia fedha hizo chuo kimeendelea kuongeza idadi ya udahili kila mwaka wa masomo.
Mahafali ya 39 yameadhimishwa sambamba ya uzinduzi wa kitabu cha historia ya chuo hicho ambao katika mahafali hayo zaidi ya wanafunzi 3800 wamehitimu katika ngazi mbalimbali zikiwemo astashada, stahaha, shahada na uzamili katika maeneo mbalimbali ya usimamizi na uendeshaji wa usafiri na usafirishaji.