Na Mwamvua Mwinyi, Kibaha,
WAZIRI wa maji, Jumaa Aweso ameshuhudia tukio la kihistoria katika utiaji saini wa kuanza, utekelezaji wa miradi mitatu ya maji yenye thamani ya zaidi ya sh.Bilioni 48 kati ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es salaam (DAWASA) na wakandarasi wa miradi hiyo ambayo itapunguza ukosefu wa maji kwenye baadhi ya mitaa na viwanda, Mkoani Pwani.
Akishuhudia zoezi la utiaji saini wa mikataba ya utekelezaji wa miradi hiyo na kuikabidhi kwa wakandarasi ,Waziri wa maji ,Jumaa Aweso (Mb) alieleza hatua hii inaonyesha ,kazi Kubwa inayofanywa na Serikali kutatua kero ya maji nchini.
Aweso alimuagiza Kaimu Mtendaji Mkuu DAWASA kuelekeza nguvu katika kutatua kero kubwa ya maji kata ya Viziwaziwa, Kibaha Mjini, na kuhakikisha waanza utekelezaji ifikapo February 2024.
Aidha wasimamie mradi wa maji kata ya Pangani ili ukamilike kwa wakati kwani wananchi wamevumilia adha ya maji kwa kipindi kirefu.
Sambamba na hilo Aweso , alikemea na kupiga marufuku kubambika bili ya maji kwa wateja ambao ni wananchi, tatizo ambalo huwa likifanywa na wasoma mita.
“Tendeni haki kwa wananchi kupata maji, na sitomvumilia Yule atakaemgambikia mwananchi maji ,sitokubali kurudishwa nyuma katika utendaji wa wizara na kazi nzuri inayofanywa na DAWASA na Rais wetu “alisisitiza Aweso.
Aweso anaeleza kwasasa wizara ya maji inakuja na mpango wa kuweka luku za maji kwa wananchi ,na hii itasaidia kuondoa ubambikizi wa billi kwa wananchi .
Hata hivyo alieleza, wizara ya maji ipo pamoja na DAWASA kwa kazi nzuri inayofanya ,na kudai DAWASA itaendelea kuwa bora kwa kufanya kazi kwa vitendo na mwaka huu wanaufunga mwaka kwa kishindo kikubwa .
Aliwasihi na kuwasisitiza , washirikiane na viongozi wa Serikali na Chama Cha Mapinduzi , madiwani,Serikali za mitaa na kwa hakika watafanikiwa zaidi ya sasa.
Kaimu Mtendaji Mkuu, Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es salaam (DAWASA) ,Kiula Kingu alieleza DAWASA imejipanga kutekeleza miradi hiyo ya maji kwa asilimia 100.
Alifafanua ,kwasasa upatikanaji wa maji Mkoani Pwani ni asilimia 86.9 na lengo ni kufikisha maji maeneo ya Mijini matarajio ni kufikia asilimia 95 na Vijijini asilimia 85.
Akielezea, kuhusu mradi wa maji Kwala ,alisema mradi wa kimkakati uliobuniwa na kusanifiwa na DAWASA ,utagharimu Bilioni 23.6 bila VAT na ukitekelezwa kwa kutumia fedha kutoka Serikali Kuu.
Kingu alieleza, mradi huu utatekelezwa na Mkandarasi wa kampuni ya China Civil Communication and Engineering Company (CCCEC) chini ya usimamizi wa wahandisi wa ndani.
“Ujenzi wa matanki 6 ya juu ya kuhifadhia maji yenye uwezo wa kuhifadhi lita milioni 1.5, Ujenzi wa kituo cha kusukuma maji chenye tenki la kupokelea maji lenye mita za ujazo 1,000 na kazi ya ufungaji wa pampu 3 za kusukumia maji na ufungaji wa mita”.
“Ulazaji wa bomba kuu la kusafirisha maji la inchi 16 na 12 kwa umbali wa kilomita 25.1 na ulazaji wa Bomba la usambazaji maji la inchi 8 na 4 kwa umbali wa kilomita 46.4.”
Kingu alieleza, mradi utakuwa na uwezo wa kusafirisha maji kiasi Cha Lita za ujazo milioni 36 kwa siku ambazo zitatosheleza mahitaji ya viwanda, Bandari Kavu na wananchi na kunufaisha wananchi takriban 7,901 wa maeneo ya Mji wa Kwala , Bandari Kavu,viwanda vikubwa na vidogo 200 ,SGR na Marshalling Yard.
MRADI WA MAJI PANGANI.
Mradi Mwingine ni wa maji Pangani ,Mamlaka ya majisafi na usafi wa mazingira Dar es salaam (DAWASA) inatarajia kutekeleza mradi wa maji katika eneo la Pangani Halmashauri ya Mji Kibaha wenye thamani ya Bilioni 8.9 ikiwa ni muendelezo wa jitihada za kuboresha huduma ya maji.
Utekelezaji wa mradi unatekelezwa kwa kutumia fedha kutoka Serikali Kuu , Mradi huu unatekelezwa na mkandarasi wa kampuni ya Shanxi Construction Engineering Corperation and Mineral Company (SCECMC)chini ya usimamizi wa wahandisi wa ndani wa mamlaka na utahusisha ujenzi wa Tanki la kuhifadhia maji la ujazo wa lita milioni 6.
Ujenzi wa kituo Cha kusukuma maji chenye tenki la kupokelea maji lenye mita za ujazo 540 na ufungaji wa pampu za kusukuma maji pamoja na ufungaji wa mita .
Ulazaji wa Bomba kuu la kusafirisha maji inchi 12 kwa umbali wa kilomita 8.8 na kazi ya ulazaji wa Bomba la usambazaji maji la inchi 12,8 na 4 kwa umbali wa kilomita 9.9.
Mradi utakuwa na uwezo wa kusafirisha maji kiasi Cha Lita za ujazo milioni 12 kwa siku ambayo ni mahitaji ya miaka 20 ijayo na kunufaisha wananchi takariban 14,868 wa maeneo ya Kibaha -Msufini,Lulanzi, TAMCO na Pangani.
MRADI WA MAJI KIBADA MPAKA CHUO CHA UHASIBU (T.I.A)
Mradi wa maji Kimbiji mpaka chuo Cha Uhasibu ,umebuniwa ili kuweza kutumia maji yaliyopatikana eneo la Kimbiji-Kisarawe II mradi huo utakuwa na uwezo wa kusafirisha maji kiasi Cha Lita za ujazo milioni 21 na kunufaisha wananchi 160,750 wa maeneo katikati ya Jiji eneo la TAZARA ,Ukonga hadi Gongolamboto .
Mradi huu utagharimu Bilioni 12.6 na utatekelezwa kwa fedha kutoka Serikali Kuu, utatekelezwa na Mkandarasi kampuni ya Shanxi Construction Engineering Corperation and Mineral Company (SCECMC)chini ya usimamizi wa wahandisi wa ndani.
Nae Mbunge wa jimbo la Kibaha Mjini, Silvestry Koka alieleza, Jimbo lina kata 14 lakini yapo maeneo ambayo yanakabiliwa na ukosefu wa maji ikiwemo kata ya Pangani na Viziwaziwa na baadhi ya mitaa usambazaji bado ni mdogo.
Alieleza,kata ya Viziwaziwa inakabiliwa na changamoto kubwa ya ukosefu wa maji kwa takriban miaka miwili sasa huku ikiwa na wakazi zaidi ya 7,000.
Mbunge huyo alifafanua kwamba , wakazi wa eneo hilo wanataabika kutumia maji ya mabwawa na visima .
Koka alimuomba Waziri wa maji Aweso kutupia jicho la huruma kwa kata hiyo baada ya kumaliza kero kata ya Pangani.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani, alhaj Abubakari Kunenge akitoa salamu za mkoa aliishukuru Serikali na Rais SamiaSuluhu Hassan kwa Nia ya kuufungua mkoa wa Pwani kiuchumi na kimaendeleo.
Alisema ,Pwani ni kinara wa uwekezaji wa viwanda, hivyo mradi wa maji Kwala utakuwa mkombozi kutatua kero ya maji kwa wawekezaji na Kongani zilizopo eneo hilo.