Na Gideon Gregory, Dodoma.
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Patrobas Katambi amesema kuwa kwa mwaka 2021/2022, jumla ya ajira zilizozalishwa nchini kutokana na uwekezaji wa serikali na sekta binafsi ni 1,226,925 ambapo wastani wa ajira 670,140 kutoka miradi ya serikali kuu, serikali za mitaa, mashirika na taasisi za umma pamoja wastani wa ajira 556,785 katika sekta binafsi.
Katambi ameyasema hayo leo Desemba 14,2023Jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari wakati akitoa maelezo kuhusiana na shughuli zinazotekelezwa na zinazoendelea kutekelezwa nchini.
Aidha ameongeza kuwa watafutakazi 578 ambapo wanawake ni 239 na wanaume ni 317 ambao wameunganishwa na fursa za mafunzo ya uzoefu wa kazi kwa kugharamiwa na Serikali.
“Utekelezaji huu ni sawa na asilimia 133 ya lengo la kuunganisha watafutakazi 435 kwa kipindi cha miezi mitano (Julai – Novemba, 2023), vilevile watafutakazi 993 wameunganishwa na fursa za ajira kwa kugharamiwa na waajiri ambayo ni sawa na asilimia 76 ya lengo la kuunganisha watafuta kazi 1,310 katika kipindi husika,”amesema.
Sambamba na hayo amesema Serikali imetoa bilioni 3.46 kwa ajili ya ukarabati wa vyuo vya Ufundi stadi na marekebisho kwa Watu wenye Ulemavu vilivyopo Saba Saba -Singida, Yombo -Dar es Salaam, Mtapika -Masasi na Luanzari- Tabora.
“Serikali imeendelea kutoa mafunzo kupitia vyuo 6 vya Ufundi Stadi na Marekebisho kwa Watu wenye Ulemavu ambavyo ni Sabasaba – Singida, Yombo Dar es Salaam, Luanzari – Tabora, Masiwani – Tanga, Mtapika – Masasi na Mirongo – Mwanza vyenye vijana wenye ulemavu wapatao 774 na kiasi cha Tsh 568 Milioni kimetumika kuwezesha mafunzo husika,”amesema.
Pia Katambi amesema serikali imeendelea kuratibu ajira za wageni ambapo jumla ya maombi 8,392 ya vibali vya kazi yamepokelewa na kufanyiwa kazi huku kati ya maombi hayo, maombi 7,729 yamekubaliwa na maombi 82 yamekataliwa kutokana na kutokidhi vigezo vya kisheria.