NA MWANDISHI WETU, ZANZIBAR.
WANACHAMA wa Chama Cha Mapinduzi wameshauriwa kuwaamini na kuwapa nafasi za kutekeleza majukumu yao Wabunge,Wawakilishi na Madiwani ili ifikapo mwaka 2025 waweze kuwatathimini na kufanya maamuzi sahihi ya kuchagua viongozi bora.
Wito huo umetolewa na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC,Idara ya Itikadi,Uenezi na Mafunzo CCM Zanzibar Khamis Mbeto Khamis,katika muendelezo wa ziara wakati akizungumza na viongozi wa majimbo ya Mkoa wa Kusini Unguja.
Alisema viongozi wa majimbo wanatakiwa kufanya kazi zao kwa ufanisi kwa lengo la kukidhi mahitaji ya wananchi, waliowachagua kuwawakilisha katika vyombo vya kufanya maamuzi.
Mbeto, amewasihi wanachama wa Chama Cha Mapinduzi kushirikiana kikamilifu na viongozi waopo madarakani kwa sasa kwani wametokana na ridhaa zao, na kwamba kipimo cha utendaji wao wa kazi zao ndio kitawafanya wadumu katika nafasi hizo au waondolewe na waliowapa ridhaa.
“ Wanachama wenzangu wa CCM nakuombeni sana tuendelee kuwapa nafasi hao viongozi wetu wafanye kazi zao, na wale wasioonekana majimboni nyinyi ndio wenye maamuzi kupitia mchakato wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
Tuna taarifa za baadhi ya Wanachama wanapita katika majimbo na kuanza kampeni huku wakibeza na kudharau kazi zinazofanywa na viongozi wao wa sasa , muda wa kusaka uongozi bado tuwape nafasi wenzetu huku tukiwatathimini kwa kina juu ya utekelezaji wa kazi zao.”, alisema Mbeto.
Alisema kuna baadhi ya majimbo bado hayafanyi vizuri kutokana na viongozi wake kupatikana kwa njia zisizofaa hali inayosababisha viongozi hao kuwa na jeuri ya fedha na kujiona wao ni bora kuliko wapiga kura na Chama Cha Mapinduzi.
“ Tumejipanga vizuri kushughulika na kila kiongozi wapo wanaodai kuwa walishinda kutokana na fedha zao hivyo tunawambia kabisa kwamba kwa awamu hii hatutojali umaarufu wa kisiasa,fedha wala cheo, kama hujatekeleza vizuri Ilani ya CCM ya mwaka 2020/2025 jina lako tunalikata”, alifafanua Katibu huyo.
Alifafanua kwamba kama kuna wanachama wanaotaka nafasi za uongozi wanatakiwa kusubiri wakati ukifika kila mwanachama mwenye sifa ataruhusiwa kuomba ridhaa ya kuchaguliwa.
Kupitia Mkutano huo, Katibu Mbeto aliwasihi wanachama hao kufanya maandalizi ya kujitokeza kwa wingi katika zoezi la uboreshaji wa uandikishaj wa daftari la kudumu la wapiga kura ili kupata wanachama wenye sifa za kuichagua CCM katika uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2025 kwa wingi kutokana na elimu iliyotolewa na Chama hicho kwa wanachama wao.
Akizungumzia miaka 60 ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964,amesema toka awamu ya kwanza hadi ya nane za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zimefanya kazi kubwa ya kuijenga nchi katika nyanja za ustawi wa kijamii,utawala bora wenye kufuata sheria,ukomavu wa kisiasa na demokrasia na ukuaji wa uchumi wa nchi.
Alieleza kuwa Serikali ya awamu ya nan echini ya Uongozi wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Mwinyi,ameenzi kwa vitendo malengo ya Mapinduzi kwa kuhakikisha wananchi wanaendelea kuwa huru huku wakipata za fursa za maendeleo katika nyanja za Elimu,Afya,Miundombinu ya Barabara za kisasa ,Uvuvi,Kilimo,Maji Safi na Salama,Michezo na miundombinu ya kisasa ya usafiri wa Anga na Baharini.
Alisema miaka 60 ni kielelezo tosha cha kujitathimini kisiasa na kiuchumi ili kufuata njia bora za kuijenga Zanzibar kiuchumi ili kwenda sambamba na kasi ya maendeleo ya nchi za visiwa zilizoendelea kiuchumi.