Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Dkt. Jim Yonazi amepokea msaada wa vitu mbalimbali kutoka Mtandao wa Polisi wanawake (TPF NET) ambao umekabidhiwa na Kamishna wa Kamisheni ya Ushirikishwaji wa Jamii CP Faustine Shilogile na Kamishna wa Utawala na menejimenti ya Rasilimali watu CP Suzan Kaganda kwa ajili ya waathirika wa maafa ya maporomoko ya matope yaliyotokea Wilaya ya Hanang mkoani Manyara.
Msaada huo wenye thamani ya shilingi milioni 17.7 umetolewa Disemba 14, 2023 katika Ofisi ndogo ya Waziri Mkuu (Ngome) Jijini Dodoma ambapo miongoni mwa vitu vilivyotolewa ni pamoja na mashuka, maji, mafuta, sabuni, mavazi, chakula na madaftali.
Akizungumza wakati akipokea msaada huo Dkt. Jim Yonazi ambaye ni Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu, amelipongeza Jeshi la Polisi kwa jitihada mbalimbali ikiwemo kuwakumbuka waathirika wa mafuriko na kwamba msaada uliotolewa na Mtandao wa Polisi wanawake utawafikia walengwa.
Mwenyekiti wa Matandao wa Polisi Wanawake ambaye pia ni Kamishna wa Utawala menejimenti ya Rasilimali watu CP Suzan Kaganda amesema Mtandao wa Polisi wanawake umeona utoe msaada kwa waathirika waliokutwa na maafa kwa ajili ya kuwafariji waathirika wa mafuriko hayo.