Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb.) amekizungumza katika mkutano baina ya Tanzania na Finland. Mkutano huo umelenga kuimarisha, kukuza na kudumisha ushirikiano katika sekta mbalimbali za kipaumbele kwa maslahi ya pande zote mbili.
Naibu Waziri katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Finland anayeshughulikia Ushirikiaano wa Maendeleo ya Kimataifa, Mhe. Pasi Hellman akichangia jambo wakati wa mkutano baina ya Tanzania na Finland, Jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba na Naibu Waziri katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Finland anayeshughulikia Ushirikiaano wa Maendeleo ya Kimataifa, Mhe. Pasi Hellman katika picha ya pamoja na wajumbe walioshiriki mkutano baina ya Tanzania na Finland .
…………………………..
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mara ya kwanza imefanya majadiliano ya kidiplomasia na Serikali ya Finland kwa lengo la kuimarisha, kukuza na kudumisha ushirikiano katika sekta mbalimbali za kipaumbele kwa maslahi ya pande zote mbili.
Pamoja na Tanzania kuwa na uhusiano mzuri na nchi za Nordic, Finland ndiyo nchi ya kwanza kufanya majadiliano ya kidiplomasia na Tanzania. Chimbuko la majadaliano hayo ni kuendelea kuimarisha ushirikiano baina ya Tanzania na nchi za Umoja wa Ulaya.
Mkutano huo kwa upande wa Tanzania umeongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb.) wakati upande wa Finland umeongozwa na Naibu Waziri katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Finland anayeshughulikia Ushirikiano wa Maendeleo ya Kimataifa, Mhe. Pasi Hellman.
Akizungumza katika mkutano uliokutanisha pande hizo mbili leo tarehe 14 Disemba, 2023 Jijini Dar es Salaam, Waziri Makamba amesema kuwa kutetea na kulinda misingi ya demokrasia na utawala bora ni kipaumbele cha Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Waziri Makamba ameeleza kuwa maboresho yaliyofanyika katika sheria ya vyama vya siasa na sheria ya uchaguzi yameleta mageuzi katika kuendesha chaaguzi mbalimbali nchini na uhuru wa vyama vya siasa kuendesha shughuli zake nchini.
Aidha, Tanzania itaendelea kulinda na kukuza misingi ya haki za binadamu, demokrasia na utawala bora kama nguzo muhimu ya kuleta maendeleo endelevu nchini.
Kwa upande wake, Naibu Waziri katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Finland anayeshughulikia Ushirikiaano wa Maendeleo ya Kimataifa, Mhe. Pasi Hellman amesema ushirikiano kati ya Finland na Tanzania umekuwa imara kwa zaidi ya miaka 50 na utaendelea kuimarika kutokana na misingi imara ya ushirikiano iliyopo baina ya mataifa hayo.
“Huu ni mkutano wetu wa kwanza wa majadiliano ya kidiplomasia kati ya Finland na Tanzania ambapo umelenga kuimarisha ushirikiano, kubadilishana ujuzi na uzoefu wa masuala mbalimbali yanayohusu diplomasia na maendeleo katika sekta mbalimbali baina ya nchi zetu”.
Kadhalika kupitia mkutano huo, viongozi hao pamoja na mambo mengine, wamejadili masuala ya biashara na uwekezaji, uwezeshaji kiuchumi, uwezeshaji wanawake, ushirikiano wa kikanda kati ya Ulaya na Afrika, kizazi cha usawa, hali ya hewa, mabadiliko ya tabianchi pamoja na masuala yanayohusu ulinzi na usalama.
Mkutano huo ulihudhuriwa na Makatibu Wakuu kutoka Wizara za Kisekta (Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Elimu, Uchukuzi, Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto, Ulinzi na Makamu wa Rais Mazingira).
Wengine ni Balozi wa Tanzania Nchini Finland, Balozi wa Finland nchini Tanzania pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC).