Mbunge wa Viti Maalum(CCM) Mkoa wa Dar es Salaam Mh.Janeth Masaburi akipata maelezo ya Mradi wa Samia Housing Scheme kutoka kwa mhandisi wa mradi huo Grace Musita alipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi huo Disemba 14, 2023.
Mbunge wa Viti Maalum(CCM) Mkoa wa Dar es Salaam Mh.Janeth Masaburi akizungumza wakati alipotembelea Mradi wa Samia Housing Scheme ili kukagua maendeleo ya ujenzi huo Disemba 14, 2023, Kushoto ni Meneja Mawasiliano wa NHC Bw. Muungano Saguya.
Meneja Mawasiliano wa NHC Bw. Muungano Saguya akifafanua jambo kwa kamati hiyo ya Siasa wilaya ya Kinondoni wakati ilipotembelea mradi huo Kawe jijini Dar es Salaam.
Mbunge wa Viti Maalum(CCM) Mkoa wa Dar es Salaam Mh.Janeth Masaburi akipata maelezo ya Mradi wa Samia Housing Scheme kutoka kwa mhandisi wa mradi huo Grace Musita alipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi huo Disemba.
……………………….
Mbunge wa Viti Maalum(CCM) Mkoa wa Dar es Salaam Mh.Janeth Masaburi amezitaka taasisi za serikali zinazohusika na ujenzi wa nyumba za makazi kama NHC kubuni majengo ya wapangaji kwa wananchi wa kipato cha chini ili kulipanga jiji la Dar es salaam.
Wito huo ameutoa leo Disemba 14,2023 wakati wa ziara ya kamati ya siasa wilaya ya kinondoni walipotembelea mradi wa Samia Housing Scheme unaojegwa na shirika la nyumba la taifa NHC Kawe jijini Dar es Salaam.
Amesema jiji la Dar es salaam ni jiji la biashara lakini limekuwa na makazi mengi holela hivyo taasisi za serikali zinapaswa kubuni miradi itakayosaidia mji kuwa na hadhi ya jiji la kibiashara na kupunguza makazi holela..
“Ni rai yangu huu ni wakati wa kuipa hadhi jiji letu taasisi za ujenzi zinapaswa kubuni majengo mazuri na kuwapangisha watu ili kusaidia kupanga jiji hasa kwenye maeneo kama Manzese,Buguruni,Kigogo na Vingunguti makazi mengi kule yapo kiholela ni hatari maana kunaweza kupata magonjwa ya mlipiko lakini hata ikitokea majanga Kam moto hakuna njia ya kupitishia magari ya kuzimia moto”amesema Masaburi.
Amesema nyumba hizo zinapaswa kuwa zenye viwango lakini kwa kuzingatia kipato cha mwananchi wa hali ya chini kwa kuwapa mikopo ya muda mrefu.
“Nakumbuka baada ya uhuru mwalimu Julius Nyerere alibuni namna ya kuboresha maisha ya watu aliwapa nyumba pale magomeni wapo watu wanaishi mpaka leo sasa niwaombe zama hizi za awamu ya sita ya Rais Dk.Samia Suluhu Hassan kupitia watendaji wake taasisi za ujenzi wa nyumba waangalie maeneo hayo ili kuboresha jiji la Dar es salaam liwe na nyumba bora na ya kisasa ndio liitwe hasa jiji la kibiashara”amesema
Kwa upande wake meneja mawasiliano wa shirika la Nyumba (NHC) Muungano Saguya amesema mradi wa kawe Samia Scheme wenye nyumba 560 mpaka sasa nyumba zote zimeshapata wanunuzi hivyo wamejipanga kuanza awamu nyingine ili kuhakikisha wanakamilisha mahitaji ya nyumba kwa wananchi.
Amesema mradi huo unatarajiwa kuwa na nyumba takribani 5000 ambazo zitajengwa katika maeneo mbalimbali nchini ambapo kwa Dar es salaam zitajengwa asilimia 50 ya nyumba hizo,Dodoma asilimia 30 na mikoa mingine asilimia 20.
“Mradi huu unaenda kuzalisha ajira nyingi kwa watanzania katika sekta ya ujenzi na uwekezaji wake ni mkubwa sana utakaofanywa kwa awamu”amesema Saguya.
Mradi wa Samia Housing Scheme unatarajiwa kujengwa nchini nzima na mpaka kukamilika unatarajiwa kutumia kiasi cha shilingi bilioni 460.