Ashrack Miraji same kilimanjaro
Katibu tawala Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro (DAS),Upendo Wella amebainisha kuwa changamoto ya wanyamapori hasa tembo kuvamia jamii zinazozunguka maeneo ya hifadhi Wilayani hapo umepatiwa ufumbuzi wa kudumu ambao utekelezaji wake utaanza hivi karibuni.
Hayo ameyasema alipokuwa mgeni rasmi akimwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Same (DC),Kasilda Mgeni kwenye uzinduzi wa ofisi ya Shirika la Kimataifa la Utunzaji Mazingira (WWF) Kanda ya Mkomazi Wilayani Same.
DAS Wella amesema serikali kwa kushirikiana na mashirika ya uhifadhi nchini wamedhamiria kumaliza kero ya wanyamapori (tembo) ambao wamekuwa wakivamia makazi ya binadamu na kufanya uharibifu kwa sababu ya kutafuta maji.
Amesema Moja ya hatua ya kutatua changamoto hiyo ni mpango madhubuti wa kuchimba visima katika maeneo ya hifadhi kuhakikisha wanyamapori hawatoki kwenda kufanya uharibifu kwenye makazi ya watu walio maeneo ya karibu na hifadhi.
“Tutoe elimu lakini pia tuweke mikakati ya kuweka visima kule hifadhini kuhakikisha hawa wanyama hawatoki nje,kiukweli sote ni mashuhuda,mvua mara baada ya kunyesha,changamoto ya tembo mimi sijaisikia” amesema Mella.
Meneja Mradi wa Shirika la WWF,Novati Kessy ametaja Moja ya hatua nyingine ya kutatua mgogoro huo ni kutoa elimu ya kujilinda pamoja na kupeleka askari wa hifadhi kwenye vijiji vinavyoathiriwa na adha hiyo ili kuimarisha doria na kudhibiti wanyamapori wasifanye uharibifu.
Afisa wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania ikolojia ya Mkomazi (TAWA),Juma Kibona amesema wameandaa andiko litakalo wawezesha kuchimba mabwawa katika hifadhi ya Mkomazi ambapo wanyama watapata maji jambo amabalo amesema ndilo litakuwa mwarobaini wa kudumu wa kero hiyo.
Hata hivyo Mwenyekiti wa Chama Cha Wafugaji Tanzania Kanda ya kaskazini (CCWT) ,Lekey Laizer amesema licha ya tembo kuathiri jamii yao hawana budi kushirikiana na mashirika hayo ya uhifadhi nchini kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu kwa sababu ulinzi ni jukumu lao wote.