NA Sophia Kingimali, DAR ES SALAAM
KATIBU wa Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara Dk. Hashil Twalib Abdallah amesema uwepo wa TEHAMA na ushirikishwaji wa wananchi umesaidia kupunguza wimbi la bidhaa bandia nchini
Hayo yamesemwa leo Desemba 12,2023, jijini Dar es salaam katika mkutano mkuu wa mwaka (AGM) wa Shirikisho la Viwanda Tanzania (CTI) baada ya kuwasilishwa kwa mada ya udhibiti wa bidhaa bandia nchini.
Amesema CTI wameamua kujadili mada hiyo kwa kina kuona nini kinasababisha uwepo wa bidhaa bandia na nini kinapelekea kuwepo kwa wingi bidhaa bandia ndani ya masoko yao ya bidhaa.
Amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk.Samia Suluhu Hassan anasisitiza kuweka mazingira wezeshi na rafiki katika ufanyaji wa biashara na uendelezaji wa viwanda katika jamii.
“Katika kufanya hivyo sera yetu ya viwanda inahitaji kuwa na ushindani ndani ya soko kwahiyo miongoni mwa vitu vinavyopelekea kutokua na ushindani halali ndani ya soko ni uwepo wa bidhaa bandia “amesema
Ameeleza kuwa CTI imedhihirisha kwamba ni miongoni mwa dhana zinazoweza kupelekea uondoshwaji,vita dhidi ya bidhaa bandia kuwa ni vita rahisi.
Ameongeza kuwa matumizi ya Tehama pamoja na mambo mengine wamejadili na kuona kitu ambacho kinaweza kupelekea bidhaa bandia kutokuwepo sokoni.
Amesema mjadala umejikita kwenye sera za viwanda,ubora wa viwanda lakini pia mjadala umejikita katika fursa zinazowezeshwa na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuendeleza sekta ya viwanda lakini pia katika upatikanaji wa bidhaa bora katika soko la bidhaa Tanzania.
Amesema wameelewa dhana nzima ya bidhaa bandia na jinsi ya kuidhibiti katika soko la bidhaa Tanzania ili mlaji aweze kupata bidhaa bora Serikali iweze kupata mapato stahiki na huduma katika jamii ziweze kuimarika.
Naye Mkurugenzi wa Kudhibiti Bidhaa Bandia kutoka Tume yaTaifa ya Ushindani ( FCC), Khadija Ngasongwa amesema Mkutano wa AGM pamoja na kujadili mambo mbalimbali lakini wanapaswa kujikita kwenye namna ya kudhibiti bidhaa bandia kwenye viwanda vyao ili kumlinda mlaji ili waweze kushindana katika soko.
Amesema mada ambayo aliwasilisha asubuhi ya leo ilikuwa na lengo la kukumbushana na kuelimisha hasa kwenye dhana hiyo ya viwanda ni wajibu wao wote.
“Taasisi za serikali zinapaswa kushirikiana na Kampuni na viwanda ili kuweza kusaidia kuumbua wafanyabiashara ambao wenye mbinu potofu kuto kutakia mema serikali yetu na viwanda vyetu,”amesema Ngasongwa.
Amesema bidhaa bandia kwa sasa nchini zipo kwa asilimia chache sana ambapo bidhaa feki ambayo imeongezeka kwa sasa ipo kwenye vipuli vya pikipiki , magari na vifaa vya umeme ndio vimejaa sana kwasababu soko limekuwa kubwa.
Kwa Upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa CTI, Leodegar Tenga amesema kikao hicho kimelenga kuzungumzia umuhimu wa kupambana na bidhaa bandia.
Amesema Viwanda ili vifanikiwe vinahitaji kuuza na kuleta ajira hivyo kama kuna bidhaa bandia viwanda havitaweza kupata faida.
Amesema viwanda vinapaswa kuzalisha bidhaa zenye ubora na viwango lakini pia kusajili bidhaa hizo ili kupunguza dhana ya bidhaa bandia pindi zinapokosa stika ya usajili.
“Sisi kama wenye viwanda ndo wenye bidhaa ndio wenye wajibu mkubwa sana kupambana na bidhaa bandia hivyo niwajibu wetu kuzungumzia swala hili ili tuweze kulitokomeza, “amesema Tenga.