Waziri wa Afya Zanzibar Mhe. Nassor Ahmed Mazrui akizungumza na Waandishi wa habari kuhusiana na maendeleo ya Afya katika miaka 60 ya Mapinduzi huko Karume house Mjini Unguja. (PICHA NA FAUZIA MUSSA -MAELEZO ZANZIBAR)
…………..
NA SABIHA KHAMIS MAELEZO
Waziri wa Afya Zanzibar Mhe. Nassor Ahmed Mazrui amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeleta mabadiliko makubwa katika Sekta ya afya ili kutoa huduma bora kwa wananchi.
Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari juu ya maendeleo ya sekta hiyo katika kuadhimisha miaka 60 ya Mapinduzi ya Zanzibar Waziri Mazrui amesema Wizara imefanikiwa kuimarisha miundombinu ya Afya na kutoa huduma za uhakika kwa wananchi wake.
Amesema Serikali imefanya mageuzi makubwa ya ujenzi wa hospital za Wilaya na Mkoa ambapo kwa sasa tayari hospitali hizo zinaendelea kuwapatia wananchi huduma zilizobora ili kuimarisha upatikaniaji wa huduma hizo kwa jamii.
Alisema Serikali imeimarisha miundombinu ya Hospitali ya Abdalla Mzee kwa kujenga chumba cha kutoa huduma za kusafisha damu kwa wagonjwa wa figo (dialysis) ili kuendana na viwango vya utoaji wa huduma katika ngazi ya Hospitali ya Mkoa na rufaa kwa upande wa Pemba.
Waziri Mazrui aliongeza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea na ujenzi wa nyumba za wafanyakazi wa hospitali hiyo ili kuwaweka karibu na eneo la kazi pamoja na kujenga maabara ya uchunguzi wa chakula, dawa na vipodozi ili kulinda afya za watumiaji.
Aidha alisema Wizara inaendelea na mikakati ya kuongeza idadi ya wafanyakazi wa afya na kufikia jumla ya wa wafanyakazi 7,640 wakiwemo wanaume 2,664 na wanawake 4,519 kwa ngazi tofauti za utendaji na utoaji wa huduma na kueleza kuwa Wizara imeshapatiwa kibali cha kuajiri wafanyakazi wengine 916wa kada mbalimbali za viapombele kwa mwaka 2023/2024.
Akizungumzia kuhusu kuwaendeleza kielimu wafanyakazi hao alisema jumla ya watendaji 553 wanaendelea na masomo wakiwemo 199 wanasomea shahada ya pili ikiwemo fani ya udaktari bingwa.
Mkutano huo na waandishi wa Habari uliofanyika Karume House ukilenga kuelezea Utekelezaji, Maendeleo na Mafanikio yaliyopatikana katika Sekta ya Afya.