Mafundi wakiendelea na ujenzi wa vyumba vipya vya madarasa katika shule ya msingi Magomeni Halamshauri ya wilaya Tunduru vinavyojengwa ili kupunguza msongamano wa wanafunzi madarasani pindi shule zitakapofunguliwa mapema mwezi ujao.
………………………….
Na Muhidin Amri,
Tunduru
HALMASHAURI ya wilaya Tunduru mkoani Ruvuma,imetenga zaidi ya Sh.milioni 56 kwa ajili ya kujenga vyumba vitatu vya madarasa na ofisi ya walimu katika shule ya msingi Magomeni kata ya Majimaji ili kupunguza msongamano wa wanafunzi darasani katika mwaka wa masomo utakaonza mwezi Januari 2024.
Hayo yamesemwa jana na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Chiza Marando,wakati akitoa taarifa ya kazi ya uboreshaji wa miundombinu ya elimu inayoendelea kufanyika kwa baadhi ya shule za msingi na sekondari wilayani humo.
Marando alisema,huo ni mwendelezo wa Halmashauri ya wilaya Tunduru wa wa kutenga fedha kila mwaka kutoka mapato yake ya ndani kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya elimu kwenye shule za msingi na sekondari zenye upungufu wa vyumba vya madarasa,ofisi za walimu na matundu ya vyoo.
Kwa mujibu wa Marando,kwa mwaka wa fedha 2023/2024 Halmashauri ya wilaya Tunduru imetenga zaidi ya Sh.bilioni 1.5 ambazo zitatumika kuboresha miundombinu ya elimu kwa kujenga matundu ya vyoo,vyumba vya madarasa na ofisi za walimu.
Kwa upande wake Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Magomeni Ezekiel Menge alisema,fedha hizo zilizotolewa na Halmashauri ya wilaya zitawezesha walimu kupata mazingira bora ya kufundishia na wanafunzi kukaa kwa nafasi darasani na hivyo kuongeza ari ya utendaji kazi kwa walimu.
Alisema,shule ya msingi Magomeni ina madarasa 4 yanatumiwa na wanafunzi 180 wakiwemo wavulana 94 na wasichana 86,wakati mahitaji halisi ni madarasa 8 ili kutosheleza mahitaji kwa wanafunzi wa elimu ya awali hadi darasa la saba.
Alisema,hali hiyo inapelekea baadhi ya vyumba vya madarasa kutumika na wanafunzi wa madarasa mawili tofauti,hivyo walimu kuhitaji kutumia nguvu kubwa katika ufundishaji ili kufikia malengo ya shule kitaaluma na wakati mwingine kukosa hata muda wa kupumzika.
Kwa mujibu wa Mwalimu Menge ni kwamba,ujenzi wa vyumba vipya vya madarasa vitasaidia sana walimu wa shule hiyo kufundisha kwa nafasi na kuwaondolea watoto changamoto ya kubanana katika chumba kimoja hali inayosababisha kukosa usikuvu wa kile wanachofundishwa na walimu wao.
Baadhi ya wanafunzi wa shule hiyo,wameiomba serikali kupitia Halmashauri ya wilaya kukamilisha ujenzi wa madarasa hayo ili waweze kuyatumia mara shule zitakapofunguliwa mwezi Januari mwakani.
Mussa Hamis alisema madarasa hayo yatakapokamilika yatawezesha kukaa kwa nafasi,ikilinganisha na sasa ambapo baadhi ya madarasa kuna wanafunzi zaidi 50 wanaotumia chumba kimoja na kudhibiti vitendo vya wizi vinavyofanywa na vijana wa mitaani.
Ester Salim,ameipongeza Halmashauri ya wilaya Tunduru kwa kuanza kujenga madarasa mapya katika shule hiyo kwani yatahamasisha wanafunzi wengi kupenda kwenda shule na kupunguza tatizo kubwa la utoro kwa sababu baadhi ya wanafunzi hawapendi kusoma kwenye mazingira mabaya.