Na Sophia Kingimali
WAZIRI wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari,Nape Nnauye amezitaka kampuni zinazoshughulika na Teknolojia ya Habari Mawasiliano(TEHAMA) kuona jinsi ya kuongeza thamani za huduma wanazozitoa hususani katika afya ili kuwafikia wananchi wa kipato cha chini.
Kauli hiyo ameiitoa Leo Disemba 8, 2023 jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na uongozi wa kampuni ya bima ya Jubilee, Airtel na Axieva kuhusu huduma mpya ya bima ya gharama nafuu inayotarajiwa kuhudumia watu zaidi ya milioni 17.5.
Asema serikali ya Awamu ya Sita imewekeza katika miundombinu ya vituo vya afya na kuhakikisha inakuwa na vifaa vya kisasa ili kurahisisha huduma ya afya kwa wananchi hususani wenye kipato cha chini.
Ili kuhakikisha kila Mtanzania wa kipato cha chini ananufaika na maendeleo yanayotendwa na serikali, kila mmoja aone namna ya kutumia teknolojia natamani kuona jinsi Tehama ikitumika kuokoa maisha ya watu na itakavyobadilisha maisha yao hususani katika huduma za afya,” amesema Nape
Amesema serikali ipo tayari kumuunga mkono mtu yeyote atakayetumia teknolojia kuokoa maisha ya watu wanyonge.
Amesema watu wengi wakiwekeza kwenye afya kupitia teknolojia watasaidia kutoa mchango kwa Wizara ya Afya na kuokoa fedha nyingi za matibabu ndio maana hata serikali imelenga kwa kila Mtanzania kupata bima ya afya kwa gharama nafuu.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Jubilee, Dk. Harold Andamson alisema bima hiyo itakuwa ya gharama nafuu na kila mtanzania ataweza kuitumia mara tu atakapolipa kupitia Airtel Money.
Pia amesema bima hiyo itatumika kwa zaidi ya vituo 642 ambavyo ni vya serikali lengo likiwa kuwafikia watu wenye kipato cha chini kuweza kunufaika na bima hiyo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Airtel Money, Andrew Rugamba amesema ushirikiano wa kampuni hizo tatu ni mkakati uliolenga kuleta mapinduzi katika mazingira ya bima ya afya kwa kutoa huduma nafuu zinazoendana na soko ambazo upatikanaji wake ni rahisi kwa Watanzania wote.