Na Sophia Kingimali,Dar es salaam.
MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Othman Masoud Othman ameyataka mataifa ya Afrika kuharakisha uwekaji wa mazingira bora ili kuwezesha ushiriki thabiti wa wanawake katika biashara ambapo itasaidia kuzalisha ajira nyingi nakufikia maendeleo endelevu.
Akizungumza leo disemba 8,2023 jijini Dar es salaam wakati akifunga kongamano la pili la wanawake katika biashara ndani ya eneo huru la biashara barani Afrika lililofanyika kwa siku tatu
amesema nchi za Afrika zinapaswa kuchukua hatua ili kuwa na mabadiliko ya haraka ya kuwawezesha wanawake kushiriki kikamilifu katika biashara ndani ya eneo huru la biashara .
” Ni muhimu kuweka mazingira bora ya biashara kupitia mfumo wa Sera wezeshi tunatambua changamoto za kipekee za wanawake katika ufanyaji biashara “amesema.
Amesema kuwa ili kukabiliana na changamoto zilizobainishwa katika nchi zote za Afrika hazina budi kuwa na dhamira ya dhati ya kutekeleza maazimio yaliyofikiwa katika majadiliano yaliyofanyika wakati wa kongamano hilo.
Aidha ameongeza kuwa kongamano hilo limetoa mwelekeo wa hatua zinazopaswa kuchukuliwa na nchi za Afrika .
“Ni imani yangu kwamba katika siku tatu za majadiliano katika kongamano hili kila mmoja ameongeza uzoefu na uelewa wa namna ya kukabiliana na changamoto zilizopo katika biashara ndani ya eneo Huru la biashara Barani Afrika”amesema
Amesema ili kukabiliana na changamoto zilizobainishwa nchi zote za Afrika hazina budi kuwa na dhamira ya dhati ya kutekeleza maazimio yaliyofikiwa katika majadiliano .
Ameeleza kuwa kukiwa na nia thabiti ya utekelezaji wa maazimio yaliyofikiwa ,kutatoa hamasa kwa nchi rafiki na washirika wa maendeleo kwa kushirikiana na Bara la Afrika ili kufikia lengo la kuwawezesha wanawake kiuchumi kupitia ushiriki wao katika biashara ndani ya eneo Huru la biashara Barani Afrika.
“Ni matumaini yangu kwamba maazimio ya kongamano hili yatakuwa chachu ya kuandaa na kutekeleza Ajenda ya Dk.Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kinara wa uhamasishaji wa ushiriki wa wanawake katika biashara ndani ya Eneo Huru la Biashara Barani Afrika”amesema
Nae Waziri wa Maendeleo ya Jamii , jinsia Wanawake na Watoto wa Serikali ya mapinduzi Zanzibar Riziki Pembe Juma amewahamasisha wanawake wafanya biashara kuendelea kuongeza kasi ya uzalishaji wa bidhaa na utafutaji wa soko la bidhaa wanazozalisha ndani na nje ya bara la Afrika.
Kongamano la pili la wanawake katika biashara ndani ya eneo huru la biashara barani Afrika limewakutanisha wadau wa sekta ya biashara kutoka nchi 55 za bara la Afrika.