SERIKALI imeipongeza Taasisi ya The Desk & Chair Foundation,Tawi la Tanzania kwa kuunga mkono jitihada za Rais Dk.Samia Suluhu Hassan,katika kutatua changamoto za elimu wilayani Ilemela.
Pongezi hizo zimetolewa leo na Katibu Tawala wa Wilaya ya Ilemela,Mariam Msengi kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya hiyo,Hassan Masala,wakati akipokea madawati 170 na miche 1,800 ya mbao,matunda na vivuli yaliyotolewa na taasisi hiyo kwa shule za msingi Songambele,Kitangiri C, Bwiru,Isanzu,Amani,
Amesema serikali inayoongozwa na Rais Dk.Samia imeweka mkazo kuendeleza sekta ya elimu kwa kujenga miundombinu ya shule,hivyo inaishukuru The Desk & Chair Foundation kwa kuguswa na kuwa mstari wa mbele kuipunguzia serikali changamoto katika sekta ya elimu ambapo madawati hayo kila moja litakaliwa na watoto watatu.
“Ni jambo la kuenziwa kwani baadhi ya shule watoto wanakaa chini juu ya sakafu,serikali ikipata fedha itaendelea kutatua changamoto hiyo na rai yangu ka wanafunzi wa shule chache zilizonufaika na madawati haya mkayatunze ili wenzenu watakaokuja wayatumie,”amesema Msengi.
Naye Mwenyekiti wa taasisi hiyo,Alhaji Dk.Sibtain Meghjee amesema wanatekeleza miradi 45 maeneo mbalimbali ukiwemo wa ukarabati wa madawati wilayani Ukerewe na hivyo madawati hayo yatapunguza adha ya watoto kukaa chini madarasani katika shule za msingi.
Amesema msaada huo mbali na watalii wengine walioshiriki kufadhili ni Aiden na Zara Ramji,Travon Muhhamad,Well Wishers na familia ya Tellis Foundation ambao ana uhakika wataendelea kusaidia kutatua changamoto za elimu zikiwemo za kijamii.
Aidha kwa niaba ya wanafunzi John Daniel ameishukuru serikali kutoa elimu bure na The Desk & Chair kwa msaada wa madawati ambao utawapunguzia adha ya kukaa chini iliyosababisha baadhi kuandika hati mbaya huku Caren Pacshal akisema utaongeza ufaulu na kukuza taaluma.
Mwenyekiti wa Kamati ya Huduma Manispaa ya Ilemela, Hussein Magera,amesema msaada wa madawati hayo 170 umeandika historia ya kupunguza sehemu kubwa ya kero ya madawati yanayohitajika,yataongeza ufanisi kwa wanafunzi kujifunza na walimu kufundishia.
Akizungumza kwa niaba ya madiwani wa kata za shule saba zilizonufaika,Diwani wa Kitangiri (CCM) Donald Ndaro amesema atakuwa mwizi na mtovu wa fadhila asipowashukuru The Desk & Chair Foundation kuwapunguzia aibu ya kukosa madawati pia kuwapa nafuu ya bajeti ya kuhudumia jamii.
“Nimewaona mkitoa misaada ya kijamii maeneo mbalimbali mkiunga mkono jitihada za Rais Samia za kumrua mama ndoo kichwani na kufanya kazi ya hamasa kwa watu wa nje.Ni akili ya ziada kutoa madawati na miche ya miti ili kurejesha uoto wa asili na mazingira,”amesema.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Ilemela,Marco Isack,ameeleza upungufu wa madawati ni 3,629 kati ya 26,444 ya mahitaji ya shule 83 za msingi,hivyo kupata hayo 170 bado wanahitaji 3,459 ambayo watayapunguza kwa fedha za mapato ya ndani kukidhi mahitaji ya shule hizo.