Na Selemani Msuya
MTANDAO wa Asasi za Kiraia za Sekta ya Maji na Usafi wa Mazingira
(TAWASANET) umetoa wito kwa serikali na wadau wengine kudumisha ushirikiano katika kuhakikisha huduma
zinawafikia waathirika wa maporomoko ya maji na matope yaliyotokea wilayani Hanang mkoani Manyara.
Aidha, TAWASANET imeeleza kusikitishwa na taarifa ya janga la mafuriko ya maji iliyoambatana na maporomoko ya udongo ambayo ambalo limeathiri taswira ya maisha ya baadhi ya wakazi wa eneo la Katesh, kukatisha uhai kwa baadhi ya wananchi, na kuharibu miundombinu mbalimbali ikiwemo ya maji na usafi wa mazingira.
Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa Bodi ya TAWASANET, Mhandisi Herbert Kashililah katika taarifa aliyoitoa kwa vyombo vya habari kwa ajili ya kutoa pole kwa Rais Samia Suluhu Hassan na wananchi wa Hanang ambao wamepatwa na janga la maporomoko ya matope na kusababisha vifo zaidi 69, majeruhi 117 na kuharibika nyumba zaidi 1,500.
Alisema TAWASANET inashauri juhudi hizo ziendelee kuratibiwa vizuri katika kuongeza tija, na hatimaye kurejesha hali ya kawaida kwa wakazi wa eneo lililo athirika.
“Pia tunatoa wito kufanya tathmini ya mapema, kutambua mahitaji halisi ya waathirika, ili kurahisisha taarifa kwa wadau wa maendeleo wakiwemo asasi za kiraia kuhusiana na mahitaji (ya muda mfupi, wa kati, na muda mrefu).
Hili litarahisisha ufanyaji maamuzi kwa wadau wa maendeleo wanaounga mkono juhudi za Serikali katika kukabiliana na janga hili,”alisema.
Mhandisi Kashililah alisema pia inapaswa kuandaa taarifa ya kina itakayosaidia kuboresha mifumo ya ufuatiliaji, utambuzi wa mapema na kukabiliana na majanga katika upande wa Sera, na uhalisia katika utekelezaji.
“Hii itasaidia namna ya kukabiliana na majanga kwa siku zijazo, endapo yatatokea ili kupunguza au kuzuia kabisa madhara kwa wananchi,”alisema
Mwenyekiti huyo alisema TAWASANET inaendelea na juhudi ya kuhamasisha asasi za kisekta na wadau wa maendeleo kwa ajili ya kukusanya na kufikisha kwa kadiri inavyowezekana mahitaji muhimu kwa waathirika.
Alisema kufanya tathmini na kuishauri Serikali namna bora zaidi ya kukabiliana na majanga kabla, wakati, na baada.
Kashililah alitoa wito kwa wadau wa maendeleo, kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali zilizopo, kufanikisha upatikanaji wa misaada ya kibinadamu kwa waathirika.
Alisema wote wana jukumu mahususi la kufanya katika kipindi hiki cha janga lililotokea, hivyo wanapaswa kuunganisha juhudi ili kuhakikisha waathirika wa janga hili wanapata huduma muhimu, ikiwemo maji safi na salama, usafi wa mazingira, na tiba.
“Tunawaombea afya njema majeruhi wote, na faraja ya Mwenyezi Mungu wale wote waliopoteza wapendwa wao wa karibu ili warejee katika hali zao na mazingira yao ya awali mapema, hatimaye kuendelea na majukumu ya kujenga Taifa letu,” alisema.
Alisema TAWASANET inatambua kwamba janga la mafuriko na madhara yake limerudisha nyuma juhudi za Serikali na wadau mbalimbali wa maendeleo katika kuhakikisha upatikanaji wa maji safi na salama kwa wakazi wa eneo husika, pamoja na huduma za usafi wa mazingira.
“TAWASANET inatambua kwamba uharibifu wa miundombinu unaongeza hatari ya kuongezeka kwa magonjwa ya mlipuko kama kipindupindu na homa ya matumbo, yanayohusiana na kuchanganyika kwa maji safi na maji taka, hivyo kuhitaji hatua za ziada kuchukuliwa kudhibiti hali hiyo.
Kashililah alisema TAWASANET inatambua na kupongeza juhudi kubwa na za haraka zilizochukuliwa na zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali katika ngazi zote ikiwa ni pamoja na kutuliza taharuki kubwa iliyosababishwa na janga hili na mipango ya huduma za dharura iliyowekwa na vyombo mbalimbali vya ulinzi na usalama kwa kuchukua hatua za haraka za uokoaji wa wahanga na waathirika wa janga hili.