OR-TAMISEMI
Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais – TAMISEMI anayeshughulikia TAMISEMI Bw. Sospter Mtwale amewataka Watendaji wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya kuimarisha utendaji kazi wao kwa kusimamia misingi ya utawala bora na kutoa huduma bora kwa wananchi.
Mtwale ameyasema hayo 05.12.2023 wakati wa ziara ya kikazi jijini humo akiwa ameambatana na Mkurugenzi wa Tawala za Mikoa na Mkurugenzi wa Serikali za Mitaa ambapo alipata nafasi ya kukutana na watumishi wa halmashauri hiyo.
Amesema watumishi tunapaswa kusimamia misingi ya utawala bora ikiwa ni pamoja na uwazi, uwajibikaji, ushirikishwaji, utawala wa sheria na ufanisi wenye tija katika kutekeleza majukumu yetu ya kila siku ili mwananchi aweze kupata huduma stahiki kutoka kwenye halmashauri yake.
Aidha Mtwale amewataka watumishi wa Jiji la Mbeya kuhakikisha wanasimamia ukusanyaji wa mapato ili shughuli mbalimbali zilizowekwa kwenye bajeti ya halmashauri zitekelezwe kikamilifu lakini pia kuongeza pato la Serikali.
Pia amesisistiza kuhusu ujibuji wa hoja za Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
“Mnajua dhahiri kuna hoja ambazo ziliwasilishwa kupitia taarifa ya CAG haitakua busara hoja hizi zikaendelea kuonekana kwenye taarifa kwa mwaka ujao. Ni jukumu la kila mmoja wetu kuhakikisha kuwa anafanyiakazi hoja inayomuhusu na kwa umoja wenu kama menejimenti muweze kuzifuta hoja hizo.
Aidha alisisitiza halmashauri hiyo kufanyia kazi maelekezo yaliyotoelwa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu ya Serikali za Mitaa (LAAC) kuhusu hoja za CAG.
“Ni matumaini yangu kila mmoja wenu anakumbuka maelekezo yale yaliyotolewa na kamati hivyo nawasisitiza mhakikishe mnayafanyiakazi kikamilifu.”
Wakati huo huo Mtwale amepongeza uongozi wa Halmashauri hiyo kwa kusimamia vyema utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa na fedha za Serikali kuu lakini pia na ile inayotekelezwa na fedha za mapato ya ndani.