Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amesema kazi ya kuondoa tope inaendelea na shughuli kubwa inayofanyika kwa sasa ni kufungua mitaa yote ya mji wa Katesh na kurejesha mji katika hali yake ya awali kwa kuwezesha shughuli za uzalishaji kuendelea.
Ameyasema hayo mapema asubuhi hii wakati wakikagua kazi zilizofanyika ambapo aliambatana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Jenista J. Mhagama, Waziri wa Madini, Antony Mavunde na Viongozi wengine , leo tarehe 6 Disemba 2023.
“Maelekezo ya Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha leo kufikia usiku, mji wa Katesh na mitaa yake iwe imesafishwa ili kushughuli za uzalishaji ziendelee kama mnavyoona Wafanyabiasha wameanza kufungua Maduka” amesema Bashungwa
Bashungwa amesema TANROADS kwa kushirikiana na TARURA tayari ameweka mpango kazi wa pamoja ambao utahakikisha kazi hiyo inaendelea kufanyika usiku na mchana mpaka shughuli hiyo itakapokamilika.
Aidha, Waziri Bashungwa amevipongeza Vyombo vya ulinzi na Usalama, kwa kazi kubwa wanayofanya ambapo wamehakikisha wanaleta vijana wa JKT wanaoshiriki katika zoezi la uokozi ikiwa ni pamoja na kusaidia kazi za kurejesha hali nzuri katika mji wa Katesh.
Naye, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Jenista Mhagama amesema kuwa wanaendelelea kutekeleza maagizo ya Mheshimiwa Rais ambayo jambo la kwanza lilikuwa ni kukabiliana na mafuriko na kuhakikisha matibabu kwa wahanga yanatolewa bure.
Amesema jambo jingine ni kuhakikisha wanaendelea kutafuta miili, kazi ambayo inaendelea na inafanywa na vikosi vya ulinzi na usalama na kuhakikisha wale ambao wanaokolewa wanatayarishiwa maeneo ya kuishi na kupatiwa huduma nyingine za kijamii.
Vilevile , Waziri Jenista ameongeza kuwa, Serikali inaendelea kupokea michango kutoka sehemu tofauti tofauti kwa ajili ya waanga wa maafa ili kuweza kuwarudisha katika hali yao ya awali.
Kazi hiyo ya kuondoa tope katika Mji wa Katesh Wilaya ya Hanang’ Mkoa wa Manyara na kurejea katika hali yake ya awali ni baada ya kuharibiwa na maporomoko ya matope kutoka Mlima Hanang’ na kusababisha madhara ikiwemo vifo, majeruhi na uharibifu wa mali na miundombinu.