Mkuu wa Mkoa wa Mjini MagharibiIdrisa Kitwana Mustafa akiwa katika picha ya pamoja na watendaji wa Ofisi ya Msajili wa hazina Zanzibar pamoja na wadau wa Uchumi na Masuala ya Kijamii( UNDESA),Mfuko wa Maendeleo ya Mitaji,(UNCDF) na Umoja wa Mataifa Ofisi ya Project Services (UNOPS) mara baada ya kufungua mafunzo ya kuwajengea uwezo wafanyakazi wa Taasisi mbalimbali za Serikali juu utanzaji wa mali za umma.
Na Rahma Khamis – Maelezo.
Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Mh, Idrissa Kitwana Mustafa amemtaka Msajili wa Hazina kuendelea kutafuta Wadau mbalimbali ambao watasaidia kuimarisha mifumo imara ya Usimamizi wa Mali za Umma.
Wito huo ameutoa katika Ukumbi wa Hoteli ya Zanzibar Beach Resort Mazizini wakati akifungua mafunzo ya kuwajengea uwezo wafanya kazi wa Taasisi mbalimbali wanaotunza mali hizo.
Amesema miongoni mwa majukumu ya ya Ofisi ya Msajili wa Hazina na Usimamizi wa Mali za Umma Zanzibar kwa mujibu wa Sheria No. 6 ya mwaka 2001ni kusimamia uwekezaji na kwa niaba ya Serikali na kusimamia mali zote za Serikali ya Mapinduzi Zanzibzr.
Aidha amesema Mafunzo hayo ni muhimu kwa watendaji wa Serikali kwani itawajengea uwezo katika usimamizi wa mali za umma na hatimae kusaidia katika kuleta maendeleo ya Taifa.
Amefahamisha kuwa mafunzo hayo yameenda sambamba na maono ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt Hussein Mwinyi ya kuhakikisha mali za Umma zinatunzwa na kutumiwa kwa malengo ili ziweze kuleta tija kwa Taasisi na Serikali kwa ujumla.
Hata hivyo Mkuu huyo amewataka watendaji kubadilika na kuwa mabalozi wazuri na kuongeza juhudi za kusimamia mali za umma katika mifumo iliyo sahihi.
“Msiwe wachoyokushirikisha wengine kutoa elimu hii ,kumbukeni kuwa kuwawezesha wengine yale mliyojifunza leo, mtakua mnazidi kuyaelewa zaidi masuala ya usimamizi ya mali za umma,aliwakumbusha.
Nae Mkurugenzi Ofisi ya Msajili wa Hazina Wahid Mohd amesema changamoto inayowakabili ni ukosefu wa mfumo ambao utasaidia kuzuwia mali za Serikali zisipotee.
Ameongeza kuwa ujio wa wataalamu utasaidia kuwafunza na kuwasadia watendaji wengine katika Serikali kwani usipotunza mali za Serikali umekwenda kinyume kwa mujibu wa sheria.
Aidha amewataka washiriki kuwa tayari kuyapokea na kuyafanyia kazi mafunzo hayo pindi mfumo utakapokuwa tayari kutumika ili uweze kuwasadia katika kazi zao.
Kwa upande wao washiriki wa mafunzo hayo wameeleza kuwa kupitia mafunzo hayo wataweza kufuatilia na kusimamia zaidi mali zote za Serikali pamoja na kufanya kazi kwa ufanisi.
“Ni wajibu wetu kutunza mali za Serikali kwani hatutoulizwa na Rais tu kama hatukutunza mali hizo,bali hata mbele ya Allah tutatulizwa kuhusu mali “walifahamisha washiriki wa mafunzo hayo.
Mafunzo hayo ya siku tatu yameandaliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Uchumi na Masuala ya Kijamii( UNDESA),Mfuko wa Maendeleo ya Mitaji,(UNCDF) na Umoja wa Mataifa Ofisi ya Project Services (UNOPS)