Na Selemani Msuya
TAASISI ya Mwalimu Nyerere (MNF) imesaini mkataba wa miaka 10 wa dola za Marekani milioni 3 na Kampuni ya Greyhorse Clearinghouse Limited ambayo ni kampuni tanzu ya Greyhorse Financial Corporation ya Marekani.
Hayo yamesema na Mkurugenzi Mkuu wa MNF, Joseph Butiku ambaye amesema lengo la mkataba huo ni kuendeleza awamu ya awali ya Makubaliano (MoU) yaliyosainiwa ambayo yamelenga kutoa mfumo wa ushirikiano kati ya taasisi hizo mbili katika utekelezaji wa mpango wa muda mrefu wa kukuza na kuimarisha uwezo wa kujitegemea wa taasisi na watu binafsi nchini Tanzania, Afrika na dunia kwa ujumla.
Alisema mkataba huo wa fedha utajikita katika kuweka mfuko wa kuimarisha taasisi zisizo na faida. “Hivyo, mkataba huu wa fedha unachukua hatua za mwanzo katika kuunda mifuko ya kudumu ya taasisi na watu binafsi kama sehemu ya mkakati wa mfuko wa kudumu kwa ajili ya kukuza na kuimarisha uwezo wa kujitegemea wa taasisi na watu binafsi,” alisema.
Mkurugenzi huyo alisema dola za Marekani milioni 3 ambazo taasisi hizo zimesaini zitakuwa zinatolewa kwa awamu ambapo kwenye kiwango cha kukuza uwezo wa kujitegemea kwa watu binafsi, lengo litakuwa ni kutenga fedha za mfuko wa kudumu katika vikundi vya jamii:
“Fedha hizo zitaelekezwa kwenye mfuko wa elimu ya watoto, walimu na Programu ya Uongozi wa Vijana wa Kiafrika wa Mwalimu Nyerere,” alisema.
Alisema mchango mkubwa wa awali kwa programu utatoka kwa Greyhorse Clearinghouse Limited ambayo itachangia jumla ya dola za Marekani milioni 3, kwa kipindi cha miaka kumi (10) na mchango wa kila mwaka utakuwa dola laki 300,000.
Butiku alisema fedha hizo zitagawanywa ambapo dola za Marekani laki 150,000, zitatengwa kwa ajili ya shughuli za utawala za taasisi na dola laki 150,000, zitaelekezwa kwenye Mfuko wa Kudumu wa Mwalimu Nyerere wa MNF.
Alisema wanufaika watakuwa watoto, vijana, kuanzia umri wa miaka 0 hadi 20 ambapo watajumuishwa katika mpango wa kudumu ambao utahakikisha uwezo wao wa kukidhi gharama zao za elimu na kuanzisha na kuendeleza biashara zao unaongezeka.
Kundi lingine la wanufaika wa mpango huo ni walimu binafsi ambao watawahamasishwa na kuwapa motisha, ili kuwawezesha kuimarisha uwezo wao wa kujitegemea katika makazi na shughuli za kiuchumi.
“Vijana wa Kiafrika watapatiwa mafunzo ya uongozi kwa njia ya mtandao kwa lengo la kukuza amani, umoja wa Kiafrika, na maendeleo yanayozingatia watu binafsi kujitegemea, ikiwa ni pamoja na mafunzo ya kuimarisha uwezo na viwango vikali vya uadilifu na tabia za maadili kwa maendeleo bora ya jamii katika bara la Afrika,” alisema.
Alisema programu hiyo itatekelezwa kupitia miradi na mikakati iliyoandaliwa kwa undani ambayo itajumuisha maeneo Mfuko wa Kudumu wa Mwalimu Nyerere, Mfuko wa Elimu ya Watoto, Mfuko wa Walimu na Programu ya Uongozi wa Vijana wa Kiafrika wa Mwalimu Nyerere kupitia mtandao.
Mfuko wa Kudumu ni juhudi kamili ya sekta binafsi iliyotokana na uaminifu wa kampuni kwa kiasi kikubwa, unashughulikia utakasishaji wa matokeo, na mbinu za kifedha zilizoimarishwa kibiashara kwa ajili ya malengo thabiti ya MNF na wadau wake wote walio hai.
Usimamizi na uendeshaji wa Mfuko wa Kudumu unafanywa na Idara ya Usimamizi wa Mali ya Greyhorse inayofanya kazi kupitia baraza lililoteuliwa la imani ya kudumu ambalo linajumuisha wataalamu waliochaguliwa kutoka kwenye taasisi.
Mchango halisi na uaminifu wa mali ni jukumu moja kwa moja la Greyhorse inayofanya kazi kupitia mitandao yake ya kifedha ya ulimwengu inayoshirikiana chini ya uongozi wa mwanzilishi na mwenyekiti mtendaji wake, Rahim Thawer, na bodi zake na kampuni zinazohusiana na mfuko za taasisi huko New York Marekani na London Uingereza.