Na Ahmed Mahmoud
Mkuu wa Mkoa wa Arusha,John Mongella amemkabidhi Mganga Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Dkt. Charles Rashid Mkombachepa, Lori la Kliniki Tembezi(mobile clinic), na kuagiza kuanza, mara moja, kufanya kazi kwenye halmashauri ya Ngorongoro.
Mongella, ameweka wazi kuwa Lori hilo tembezi, limeletwa kwa ajili ya kutumiwa na Madaktari Bingwa kutoa huduma kwa wagonjwa walio kwenye maeneo ya pembezoni, ambayo hayafikiki kwa wepesi.
Mongella, hakusita kumshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuwajali wananchi wa Arusha, ambao Jiografia ya maeneo yao hayafikiki kwa wepesi na watu wake wanaishi kwa mtawanyiko mkubwa, ambao wanahitaji huduma za afya.
Amesisitiza Mganga Mkuu wa mkoa kuhakikisha anawapangia Madaktari Bingwa, kwenye halmashauri za pembezoni kwa kuanza na wilaya ya Ngorongoro, Longido na baadhi ya maeneo ya wilaya ya Arumeru, ambapo Jiografia ya maeneo yake haifikiki.
Ameagiza Lori hilo tembezi, kuanza kazi kwenye wilaya ya Ngorongoro na madaktari walifuate gari hilo, huko huko ili madakatari hao watoe huduma kwa wananchi.
Kwa Upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Arusha amepokea maagizo hayo na kueleza ataànda ratiba ya shughuli za gari tembezi la matibabu wilayani Ngorongoro haraka iwezekanavyo.
Nae Mbunge wa Ngorongoro amesema kwamba yapo maeneo ambayo sio rahisi kufikika ndani ya wilaya hiyo hivyo wanamchukuru Rais Samia kwa kuwaletea huduma hiyo ya gari tembezi na kuahidi kufuatilia kwa karibu ili malengo ya uwepo wa klinik hiyo tembezi yanafanikiwa na wananchi wanapata huduma hiyo.
Jumla ya Magari matatu ikiwemo Ambulance mbili ambazo zimegawiwa kwa halmashauri za Ngorongoro na Longido sanjari na Kliniki tembezi Moja yamekabidhi na Mkuu wa Mkoa wa Arusha John Mongella kwa viongozi wa wilaya hizo mbili.