Na Mwandishi Wetu
Benki ya NMB imenyakua tuzo nne kwenye shindano la mwaka huu la Mwajiri Bora wa Mwaka (EYA 2023), ukiwemo ushindi wa pili kwenye mshindi jumla wa tuzo hizo zilizoandaliwa jana jijini Dar es Salaam na Chama cha Waajiri Tanzania (ATE).
Tuzo nyingine ilizoshinda benki hiyo ni za mshindi wa pili wa Sekta Binafsi, wa kwanza katika Ubora, Tija na Ubunifu, na wa kwanza pia kwenye Masuala ya Usawa wa Kinjinsia.
Hii ni mara ya pili mfululizo kwa benki hiyo kung’ara kwenye tuzo hizo za kila mwaka baada yakutangazwa kuwa Mwajiri Bora wa Mwaka 2022 na kushinda tuzo nyingine mbili kutokana na ubora wake wa kibiashara na katika usimamizi wa rasilimali watu.
Tangu mwaka 2005, ATE imezitumia tuzo hizi kuyahamasisha na kuyatunuku mashirika yanayozingatia maslahi na maendeleo ya watumishi katika shughuli zake. Waajiri wamekuwa pia wakitambuliwa kwa kuwa na sera zinazozingatia ushindani wa kitaasisi, ubora wa kitija pamoja na uwepo wa amani na utulivu sehemu za kazi.
Akizungumza katika hafla hiyo, Afisa Mkuu wa Rasilimali Watu wa NMB, Bw Emmanuel Akonaay, alisema tuzo za ATE walizoshinda ni miongoni mwa tuzo nyingi za ufanisi na ubora za kitaifa na kimataifa ambazo imezinyakua NMB mpaka sasa mwaka huu.
Kiongozi huyo aliongeza kuwa tuzo hizo pamoja na ufanisi wa utendaji kifedha uliopatikana mwaka huu hususani faida kubwa iliyopatikana umeufanya mwaka 2023 kuwa mwaka mwingine wa mafanikio makubwa kwa benki hiyo kubwa kuliko taasisi zote za fedha nchini.
“Tuzo hizi pia ni ishara kuwa imani kubwa kwa Benki yetu sio tu kwa wateja wetu lakini zaidi kwa wafanyakazi waliopambana mpaka kufikia hatua hii kubwa ya mafanikio. Wafanyakazi wetu wana imani kubwa na sisi, wanaupendo na Benki yetu na ndio maana wanafanya kazi kwa juhudi kubwa mpaka kunatunukiwa tuzo hizi,” Bw Akonaay alibainisha.
Aidha, alisema hivi karibuni benki hiyo pia ilitunukiwa tuzo ya mlipa kodi mkubwa nchini na ile ya taasisi inayoongoza kwa kuzingatia misingi na kanuni bora za ulipaji kodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
“Hii inathibitisha namna ambavyo Benki ya NMB inashirikiana vyema na Serikali pamoja na mashirika yake,” Bw Akonaay aliwaambia waliohudhuria shughuli hiyo akiwemo Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu), Prof Joyce Ndarichako, aliyemwakilisha Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.
Pia Bw Akonaay alisema NMB imenufaika sana na tuzo hizo za ATE hasa katika kuihamasisha kuwekeza zaidi katika kuwaendeleza wafanyakazi wake na kuweka mazingira rafiki ya kazi kama inavyoelekeza Serikali.
Aliongeza kuwa NMB si tu ina wafanyakazi wengi bali pia inazingatia usawa wa kijinsia kazini ambapo kwa sasa wanawake ni asilimia 48 ya wafanyakazi wake wote huku wanaume wakiwa ni asilimia 52.