Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Ushirikiano wa Elimu Duniani (GPE), Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, pamoja na Makamu Mwenyekiti wake Susan Liautaud na Afisa Mtendaji Mkuu wa GPE, Bibi Laura Frigenti, leo wametembelea na kukagua skuli ya Maandalizi ya Kikaangoni wilaya ya Magharibi mkoa wa Mjini Magharibi leo.
Dkt. Kikwete, akiwa mwenyekiti wa GPE ataongoza vikao vya Bodi vya Shirika hilo hapa Zanzibar kuanzia leo tarehe 4 hadi 6 Disemba, hiyo ikiwa ni mara ya kwanza kwa Shirika hilo la kimataifa kufanya vikao vyake vya bodi barani Afrika..
GPE iliyoanzishwa mwaka wa 2002, ni Shirika linalosimamiwa na Benki ya Dunia, linalofadhili maendeleo ya elimu ya msingi na utendaji wa sera za nchi zinazoendelea.
Majukumu ya GPE ni pamoja na kusaidia serikali za nchi zinazoendelea kufanya mabadiliko ya kimfumo na kuoanisha rasilimali na ufadhili ili kutoa elimu bora kwa watoto Wote, kuinua viwango vya kujifunza na kukabiliana na changamoto mpya nchini.
Kwa mujibu wa Dkt. Kikwete, ambaye ni Mwafrika wa kwanza kuongoza GPE, shirika hilo hadi sasa limeishaipatia Tanzania jumla ya Dola za Kimarekani Milioni 332 (takriban shilingi 834,980,332,000.00) ili kusaidia sekta ya elimu bara na visiwani.
Majuzi GPE imetiliana saini na Serikali ya makubaliano ya kutoa dola za Kimarekani milioni 85 (takriban shilingi 213, 775, 085, 000.0) kwa ajili ya kusaidia mafunzo ya walimu nchini.