Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Prof. William Mwegoha, akihutubia hadhara iliyohudhuria Sherehe za Mahafali ya 22 ya Chuo Kikuu Mzumbe, Ndaki ya Mbeya.
Rasi wa Chuo Kikuu Mzumbe Ndaki ya Mbeya, Prof. Henry Mollel, akiwahudhurisha wahitimu wakati wa Sherehe za Mahafali ya 22 ya Chuo Kikuu Mzumbe, Ndaki ya Mbeya.
Kaimu Naibu Makamu Mkuu wa Chuo – Taaluma, Utafiti na Ushauri wa Kitaalamu, Dkt. Eliza Mwakasangula, akizungumza wakati wa Sherehe za Mahafali ya 22 ya Chuo KIkuu Mzumbe Ndaki ya Mbeya.
Maandamano ya kitaaluma kuelekea uwanja wa mahafali, wakati wa Sherehe za Mahafali ya 22 ya Chuo Kikuu Mzumbe Ndaki ya Mbeya.
……..
Rais Mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ambaye pia ni Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein ameutaka Uongozi wa Chuo Kikuu Mzumbe kufanya uwekezaji katika maendeleo ya kitaaluma ikiwemo kuharakisha maendeleo ya chuo kwa kujenga mahusiano na taasisi za elimu za ndani, Afrika Mashariki na nchi za jirani ili kujiimarisha na kuongeza ufanisi katika utendaji,
Akizungumza Mkoani Mbeya Novemba 30, 2023 katika Mahafali ya 22 ya Chuo Kikuu Mzumbe Ndaki ya Mbeya, Viwanja vya Wangari Maathari Courtyard ambapo wahitimu 1,295 katika ngazi mbalimbali za kitaaluma wakiwemo Astashahada, Stashada, Shahada ya Kwanza/ Awali na Shahada za Umahiri walitunukiwa stahili zao, Mhe. Dkt. Shein, ameushauri uongozi wa chuo kuzidisha kiwango cha ushirikiano na sekta binafsi na mashirika ya umma ili kugundua changamoto zao ambazo wanaweza kuzitatua kwa kununua matokeo ya utafiti na shauri za elekezi za kitaalamu ili ziwasaidie kuimarisha bidhaa na huduma zao.
Mhe. Dkt. Shein amesema kuwa kupitia tafiti chuo kitaanzisha na kuwa na chanzo cha fedha kwa kutumia mbinu hizo kitakuwa kimeisaidia serikali katika kuleta maendeleo kwa wananchi wake.
Mhe. Dkt. Shein amesema kuwa wakati umefika wa Chuo kuwa wabunifu katika ulimwengu wa sasa unaobadilika kwa kasi.
Amesema kuwa chuo inapaswa kubuni mbinu mbalimbali zitakazowezesha kwenda sambamba na matakwa ya maendeleo ili kuinua sifa ya chuo na kuweza kuinua maisha na hadhi ya watu wanaohudumiwa.
Ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mkazo mkubwa na kipaumbele katika sekta ya elimu hapa nchini kwa kendelea kuboresha miundombinu ya chuo Kikuu Mzumbe.
“Fanyeni tafiti na kubuni teknolojia mpya ambazo zitaendana na wakati wa sasa, ajira zina ushindani na wasomi wanaongezeka, serikali imetimiza wajibu kwa kuweka miundobinu katika vyuo vya elimu ya juu, kujiamini na kujituma ndio siri ya maendeleo na dunia ya sasa, inahitaji kupambana kwani ajira ni za kupambania hivyo jiongezeeni elimu ili kufungua milango mingine,”amesema Dkt. Shein.
Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu Mzumbe Prof. Saida Yahya- Othman amewaasa wahitimu kutumia maarifa waliyopata kuwa wabunifu pamoja n kufanya kazi kwa bidii.
Amewakubusha kuongeza maarifa kwa kufanya tafiti, kutafakari pamoja na kuchambua kwa wakizingatia ukweli bila kuyumbishwa na mtu yoyote katika kutekeleza.
Amesema wahitimu wanapaswa kuishi kwa kipato halali bila kuvunja sheria pamoja na kutojihusisha na matendo maovu.
Awali Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo, Profesa William Mwegoha akizungumzia upande wa Taaluma amesema kuwa kwa mwaka wa masomo wa 2022/23, Chuo kilisajili jumla ya wanafunzi 13,718 kuanzia ngazi ya Astashahda hadi Shahada ya Uzamivu.
Amesema kuwa kati yao 8,608 walisajiliwa katika Kampasi Kuu; 3,411 Ndaki ya Mbeya na 1,699 Ndaki ya Dar es Salaam, huku baadhi ya hao,
Kwa upande wa utafiti na kujenga uwezo wa wanataaluma, katika mwaka wa masomo wa 2022/23, Chuo kimeendelea kutekeleza jumla ya miradi 17 ya Utafiti inayofadhiliwa na wadau mbalimbali wa maendeleo katika maeneo mbalimbali ikiwemo afya, Elimu, sayansi na Teknolojia, Biashara na Ujasiriamali kwa vijana, Uchumi, Sheria na Haki za Binadamu, pamoja na Miradi saba ya utafiti inayofadhiliwa na Chuo.
Akizungumza kuhusu Ushirikiano na Taasisi na Vyuo Mbalimbali Ndani na Nje ya Nchi, Prof. Mwegoha amesema kuwa kuwa Chuo Kikuu Mzumbe katika kuboresha ushirikiano wake na Taasisi za Elimu ya Juu na Mashirika mbalimbali ya kimataifa, kimejipanga kupanua wigo wa ushirikiano na Taasisi na Mashirika mya Kimataifa, kama sehemu ya kutekeleza Dira ya Chuo.
Prof. Mwegoha amesema kuwa Chuo Kikuu Mzumbe kimeendelea kutekeleza miradi ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu kama Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi kwa Tanzania (Higher Education for Economic Transformation, (HEET)) ambao unafadhiliwa na Benki ya Dunia kama mkopo kwa Serikali ya Tanzania.
“Tayari tumeanza utekelezaji wa mradi huu ambao lengo lake ni kuboresha mazingira ya kufundishia na kuhakikisha kuwa programu katika Vyuo Vikuu zinaendana na soko la ajira.
Chuo Kikuu Mzumbe kimetengewa Dola za Kimarekani milioni 21 kwa ajili ujenzi wa majengo ya kufundishia ambapo miradi hii inachukua 79.2% ya fedha zote za mradi, kupitia mitaala na kutengeneza mitaala mipya inayoendana na soko la ajira.
Chuo kina mpango wa kuboresha miundombinu ya TEHAMA, uhusiano wa Chuo na wadau wa nje, Kuwajengea uwezo wafanyakazi wa Chuo kwa kuwapatia mafunzo ikiwa ni pamoja na kuanzisha Kampasi Mpya Tanga.
Katika mafali hayo wahitimu 1,295 katika ngazi mbalimbali za kitaaluma wakiwemo Astashahada, Stashada, Shahada ya kwanza/Awali na Shahada za Umahiri walitunukiwa stahili zao.