Afisa Biashara Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) Bw. Kezilahabi Jumanne (kulia) akizungumza jambo na jamii ya wamasai katika Shamba CanBe la kunenepesha Ng’ombe katika Kijiji cha Mazizi, Kata ya Msata, Wilaya ya Chalinze, Mkoani Pwani wakiwa na wahariri wa vyombo vya habari kwa ajili kuangalia mradi wa shamba la kunenepesha ng’ombe iliyofanyika Novemba 30, 2023.
Wahariri wa vyombo vya habari wakiwa katika Shamba CanBe la kunenepesha Ng’ombe katika Kijiji cha Mazizi, Kata ya Msata, Wilaya ya Chalinze, Mkoani Pwani wakiwa katika ziara ya kuangalia mradi wa shamba la kunenepesha ng’ombe iliyofanyika Novemba 30, 2023.
Meneja Mawasiliano na Masoko wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (wapili kulia) akiwa katika picha ya pamoja na jamii ya kimasai katika Shamba CanBe la kunenepesha Ng”ombe katika Kijiji cha Mazizi, Kata ya Msata, Wilaya ya Chalinze, Mkoani Pwani.
Ng’ ombe wa nyama wakiwa katika shamba CanBe la kunenepesha katika Kijiji cha Mazizi, Kata ya Msata, Wilaya ya Chalinze, Mkoani Pwani.
………
NA NOEL RUKANUGA, PWANI
Kampuni ya CanBe Shamba la kunenepesha Ng”ombe wa nyama imeipongeza Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) kwa kufanya uwezeshaji wa maboresho ya miundombinu ya mifugo ambayo imeleta tija kwa kubadilisha maisha ya watu kiuchumi katika Kijiji cha Mazizi, Kata ya Msata, Wilaya ya Chalinze Mkoani Pwani.
Uwezeshaji uliofanywa na Benki ya TADB wametoa mkopo wa zaidi ya shillingi bilioni 1.5 kwa Kampuni ya CanBe Shamba la Unenepeshaji Ng”ombe pamoja na jamii ya kimasai ambao umekuwa msaada wa kunenepesha Ng’ombe na kuwa na uzito kuanzia kilo 150.
Akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari Novemba 30, 2023 wakiwa katika mradi wa Shamba la kunenepesha Ng’ombe katika Kata ya Msata, Wilaya ya Chalinze, Meneja wa CanBe Shamba la kunenepesha Ng’ombe wa nyama Bw. Ephantus Mwangi, amesema kuwa benki ya TADB imewasaidia kuwakopesha mtaji wa kununua ng’ombe pamoja na kutengeneza miundombinu ya ufugaji.
Bw. Mwangi amesema kuwa benki ya TADB imewasaidia kufanya ufugaji wa kunenepesha ng’ombe kisasa, kwani awali walikuwa wanafuga kienyeji ambapo ng’ombe walikuwa na uzito mdogo wa kilo 70.
“Kwa sasa tunachinja ng’ombe 10, awali kabla ya Benki ya TADB kuja tulikuwa tunachinja ng’ombe 5, tumepiga hatua kubwa katika kazi yetu na soko letu lipo Dar es Salaam” amesema Bw. Mwangi.
Amefafanua kuwa shamba hilo linaukubwa wa heka 1,000, huku akieleza kuwa wakati wanaaza kufuga walikuwa hawapati faida kutokana na gharama kubwa za uendeshaji ikiwemo kununua majani, lakini kwa sasa wameweza kuwa na shamba la majani kwa ajili ya malisho ya kunenepesha ng’ombe wa nyama.
Afisa Biashara Benki ya TADB Bw. Kezilahabi Jumanne, amesema kuwa kuanzia mwaka 2020 wameaza kutoka mkopo kwa nyakati tofauti kwa wakulima katika shamba la kunenepesha ng’ombe wa nyama ili kuongeza ufanisi.
Bw. Jumanne amesema kuwa awali walitoa mkopo wa shillingi milioni 320 kwa ajili ya maboresho ya shamba pamoja shillingi milioni 810 kwa watu nane jamii kimasai kwa ajili ya kununua ng’ombe kutoka kwa wafugaji wadogo.
“Katika shamba hili watu wa jamii kimasai wameingia mkataba na miliki wa shamba kwa ajili ya kunenepesha ng’ombe zao na baadaye kumuuzia kwa ajili ya kwenda kuuza Dar es Salaam” amesema Bw. Jumanne.
Amesema kuwa pia katika shamba la malisho ya kunenepesha ng’ombe wa nyama wametoa shilingi milioni 650 ili kupunguza gharama za uendeshaji hasa kununua malisho kutoka sehemu nyengine.
“Benki ya TADB tunafika sehemu yoyote ikiwemo zile ambazo hazifikiki kutokana na changamoto za miundombinu ya barabara, lengo ni kuwasaidia wakulima katika kuboresha maisha kupitia shughuli zao za kilimo” Bw. Jumanne.
Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) ilianzishwa chini ya Sheria ya Kampuni, 2002 CAP 212 mnamo Septemba 2012.
Miongoni mwa majukumu ni kuongoza mikakati ya kujenga uwezo na mipango ya kuimarisha mnyororo wa thamani ya kilimo na kuunga mkono Serikali ya Tanzania miradi ya kuunda na kutekeleza sera na mikopo ya kilimo na vijijini.
Mipango thabiti ya Benki ya TADB kutoa huduma za kifedha kwa kupitia kongani na minyororo ya thamani kwa nia ya kuleta mapinduzi ya kimkakati katika kilimo na kwa wakulima wadogo.