Na Sophia Kingimali
Rais Dk.Samia Suluhu Hassan anatarajia kufungua Mkutano wa kwanza wa kitaifa wa Dira ya Maendeleo ya Taifa utakaofanyika Disemba 9 mwaka huu katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) na kutumia siku hiyo kutoa ujumbe maalum katika maadhimisho miaka 62 ya uhuru.
Akizungumza leo Disemba 1, 2023 jijini Dar es Salaam na waandishi wa habari Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo amesema jumla ya wadau 971 wamealikwa kushiriki katika mkutano huo ambapo wadau kutoka pande zote mbili za muungano watahudhuriwa na makundi maalum pamoja na viongozi mbalimbali.
Amesema lengo kuu la mkutano huo ni kuzindua, kupokea na kujadili taarifa ya kitafiti ya tathimini ya utekelezaji wa dira ya maendeleo ya Taifa 2025.
“Dk. Samia atazindua rasmi timu kuu ya kitaalam ya dira na kamati ya usimamizi wa dira pamoja na nyenzo za kidigitali zitakazotumika katika kukusanya maoni ya wadau, “amesema Profesa Mkumbo.
Amesema taarifa ya kitafiti ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 pamoja na mengine pia imeainisha mafanikio yanayopatikana na changamoto zilizojitokeza katika utekelezaji wa dira hiyo.
Aidha Amesema kuwa Dira hiyo ilianza kutelezwa mwaka 2000 na inafikia mwisho wake mwaka 2025 pamoja na mafanikio mengine taarifa ya tathimini inaonesha pato la mtanzania limeongezeka kutoka Dola za Kimarekani 399.5 mwaka 2000 hadi kufikia dola 1200.
“Tanzania imefikia asilimia 124 ya kujitosheleza kwa chakula ilikulinganishwa na lengo la kufikia asilimia 140 ifikapo mwaka 2025 na kupunguza vifo vinavyotokana na uzazi kutoka vifo 760 kwa vizazi hai 100,000 mwaka 2000 hadi kufikia 104 mwaka 2022 ikiwa tumevuka lengo la kufikia vifo 265 ifikapo mwaka 2025 ni matokeo kamili ya tathimini hii,”amesema.
Ameongeza kuwa wameanza mchakato wa kuandaa Dira mapya Maendeleo ya 2050 na ametoa rai kwa wananchi kufuatilia mchakato huo na kushiriki kikamilifu katika kutoa maoni yao kuhusu Tanzania waitakayo katika miaka ijayo.