Mkurugenzi Idara ya Kinga na Elimu ya Afya Zanzibar Dkt.Salim Slim akitoa taarifa Kwa vyombo vya habari kuhusiana na zoezi la chanjo dhidi ya ugonjwa wa saratani ya mlango wa kizazi inayoenda kutolewa kwa wasichana wenye umri wa miaka 14 katika skuli zote Unguja na Pemba ifikapo Disemba 1-2 mwaka huu.
PICHA NA FAUZIA MUSSA –MAELEZO
…….
Na Fauzia Musa , Maelezo Zanzibar
Mkurugenzi Kinga na Elimu ya Afya Zanzibar Dk Salim Slim amewataka Wazazi, walezi na walimu wakuu kushirikiana ili kufanikisha zoezi la utoaji wa chanjo ya kinga dhidi ya Saratani ya Shingo ya mlango wa kizazi kwa wasichana wenye umri wa miaka 14 katika skuli zote Unguja na Pemba.
Akitoa taarifa kwa Waandishi wa habari kuhusiana na zoezi hilo huko Ofisini kwake Mnazimmoja Mjini Unguja Dkt Salim amesema kukamilika kwa zoezi hilo kutasaidia kupunguza tatizo hilo Nchini.
Alisema zoezi hilo linatarajiwa kufanyika Disemba 1 na 2 mwaka huu katika Skuli zote Unguja na Pemba na kuwasisitiza walimu na wazazi kuwahimiza wasichana hao kushiriki katika zoezi hilo kutokana na baadhi ya skuli kufungwa.
Alifahamisha kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imehakikisha chanjo hiyo kuwa ni salama na haina madhara na imethibitishwa na Shirika la Afya Ulimwenguni WHO ambayo itatolewa katika mikoa yote ya Tanzania kwa lengo la kukinga Afya za Wasichana .
Dkt. Salim ameeleza kuwa Serikali kupitia Wizara ya Afya ilizindua rasmi chanjo dhidi ya ugonjwa wa saratani ya mlango wa kizazi Aprili 19,2018 kwa lengo la kuwakinga wanawake na wasichana dhidi ya ugonjwa huo visiwani Zanzibar.
Chanjo hiyo itasimamiwa na Wizara ya Afya kupitia Mradi wa MCGL unatekelezwa na JAHPIEGO kwa ufadhili wa shirika la Msaada la Marekani USAID.