Na Sixmund Begashe
Timu ya Wataalam wa Benki ya Dunia ikiongozwa na Msimamizi Mkuu wa Mradi wa Kuboresha Usimamizi wa Maliasili na Kukuza Utalii (REGROW) wa Benki ya Dunia, Dkt. Enos Esikuri imefika katika Vijiji vilivyopakana na Hifadhi ya Taifa ya Milima ya Udzungwa na katika Hifadhi hiyo yenye vivutio vya kipekee Duniani, kwa lengo la kujionea utekelezaji wa mradi huo.
Baada ya kutembelea ujenzi wa mradi wa njia ya juu ya Miti ya kupanda na kushuka Mlima, timu hiyo ikiwa imeongozana na Wataalam wa utekelezaji wa Mradi huo hapa nchini, ilikutana na vikundi vya Kijamii (COCOBA) vinavyowezeshwa na Mradi wa REGROW katika Kijiji cha Msufini, Mang’ula B. ili kujua maendeleo ya vikundi hivyo na changamoto wanazokutananazo.
Akizungumza na Vikundi vya COCOBA kwenye vijiji hivyo, Msimamizi Mkuu wa mradi wa REGROW Benki ya Dunia Dkt. Enos Esikuri amevipongeza vikundi vyote kwa matumizi mazuri ya fedha walizopatiwa na Mradi wa REGROW kwa maendeleo ya Uhifadhi, Utalii, Familia zao na ya Jamii kwa ujumla.
Katika vikao hivyo, Wanavikundi wameupongeza uongozi huo wa Benki ya Dunia kwa kuwatembelea ili kuona maendeleo ya vikundi vyao huku wakiueleza uongozi huo, namna walivyonufaika na mradi huo, hususani kiuchumi, elimu, uwelewa mpana juu ya umuhimu wa uhifadhi wa Maliasili pamoja na kuhimarika kwa mahusiano ndani ya familia.
Mradi wa REGROW unaotekelezwa na Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kushirikiana na wadau mbalimbali maendeleo ya uhifadhi unatekelezwa kwa mkopo wa masharti nafuu ya Benki kutoka Dunia ili kuinua sekta ya Utalii na Uhifadhi endelevu Kusini mwa Tanzania.