Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb.) akiwasilisha hotuba yake katika mahafali ya 26 ya Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa cha Dkt. Salim Ahmed Salim Jijini Dar es Salaam
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb.) akimkabidhi cheti mmoja kati ya wahitimu wa Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa cha Dkt. Salim Ahmed Salim wakati wa Mahafali ya 26 ya Kituo hicho Jijini Dar es Salaam
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb.) katika picha ya pamoja na baadhi ya wakufunzi wa Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa cha Dkt. Salim Ahmed Salim Jijini Dar es Salaam
…………………………
Serikali imekitaka Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa cha Dkt. Salim Ahmed Salim kuhahikisha kinaendelea kutoa elimu bora ya Uhusiano wa Kimataifa, Diplomasia na Stadi za Stratejia.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb.) ambaye alimwakilisha Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb.) ametoa agizo hilo katika mahafali ya 26 ya Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa cha Dkt. Salim Ahmed Salim na kuwatunuku vyeti wahitimu 1,008.
Wahitimu hao wamwtunukiwa vyeti katika maeneo ya Uhusiano wa Kimataifa na Diplomasia, Diplomasia ya Uchumi, Usimamizi wa Amani na Migogoro na Utawala wa Kimkakati.
“Wizara inapenda kusisitiza umuhimu wa Kituo kuendelea kuelimisha Taifa kupitia mijadala na makongamano kwa lengo la kupanua uelewa wa masuala mbalimbali. Kituo kinapaswa pia kuendelea kusimamia na kutekeleza Majukumu ya Msingi ya kuanzishwa kwake ambayo yanajumuisha Taaluma, Utafiti na Ushauri Elekezi,” alisema Balozi Mbarouk.
Balozi Mbarouk aliongeza kuwa ni vyema Kituo kikaboresha progamu zake ili kukidhi mahitaji ya Wizara, Nchi na watanzania kwa ujumla wake, ambapo alishauri kuwa Kituo kiendelee kutoa elimu ya masuala mbalimbali yanayohusiana na Uhusiano wa Kimataifa, Diplomasia ya Uchumi na Stratejia kwa taasisi za Serikali na sekta binafsi ili kusaidia kukuza ujuzi wa wananchi wetu.
“Naelekeza usimamie utekelezaji wa mabadiliko yanayoendelea kama ilivyopendekezwa na Kamati ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kutathmini utendaji kazi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na taasisi zilizo chini yake,” Aliongeza Balozi Mbarouk.
Kadhalika Balozi Mbarouk aliwasihi wahitimu kutambua kuwa soko la ajira serikalini na sekta binafsi kwa sasa ni ngumu, hivyo watumie ujuzi na elimu waliyoipata kujiajiri.
“Maarifa mliyoyapata ni mtaji mzuri kwenu unaowapa mwanga wa kutumia fursa za ndani na nje ya nchi katika kufanya biashara na kutoa huduma mbalimbali kwa mujibu wa kile mlichosomea,” alisema Balozi Mbarouk.
Kwa Upande wake Dkt. Reweta Wande ambaye alimwakilisha Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa cha Dkt. Salim Ahmed Salim, Balozi Ramadhani M. Mwinyi, amesema Kituo kinaendelea kutoa elimu Uhusiano wa Kimataifa na Diplomasia ya uchumi pamoja na Stadi za Stratejia ambapo jitihada hizo zimetoa matunda ya ongezeko la wahitimu 1,008 kwa mwaka 2023 ikilinganishwa na wahitimu 990 kwa mwaka 2022.
“Lengo la kuanzishwa kwa Kituo ni kutoa elimu ya masuala ya Diplomasia kati ya Tanzania na Msumbiji. Ila kwa sasa Jukumu la Kituo ni kukuza maendeleo, ufahamu na uelewa wa masuala ya Uhusiano wa Kimataifa katika ngazi za kikanda na kimataifa kwa wataalamu wanaoendelea na wanaochipukia na umma kwa ujumla,” alisema Dkt. Wande
Pamoja na mambo mengine, Dkt. Wande ameahidi kuwa Kituo kitaendelea kutoa elimu ya masuala mbalimbali yanayohusiana na Uhusiano wa Kimataifa, Diplomasia ya Uchumi na Stratejia kwa taasisi za Serikali na sekta binafsi ili kusaidia kukuza ujuzi wa wananchi kwa ujumla.