Na OR-TAMISEMI, MTWARA
Watendaji wa Kata na Maafisa Tarafa wameaswa kubuni na kupanga mipango ya shughuli za maendeleo inayoleta tija kwa jamii na kuwa kiungo bora kati ya Serikali Kuu na Mamlaka za Serikali za Mitaa kwenye maeneo yao.
Akifungua mafunzo hayo ya siku mbili leo tarehe 29 Novemba, 2023 katika Manispaa ya Mtwara Mikindani kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mhe. Kanali Ahmed Abbas Ahmed, Mhe. Lauteri Canoni Mkuu wa Wilaya ya Masasi amewaasa watendaji hao kuwa wabunifu katika kupanga miradi ya maendeleo ngazi ya Kata na Tarafa, kushirikisha wananchi kwenye miradi ya mandeleo na kuwatumia Maafisa wa Serikali wa kada husika kuwahudumia wananchi.
“majukumu yenu ninyi ni kuwahamasisha wananchi katika shughuli za maendeleo, kushiriki na kutoa ushauri mzuri katika upangaji wa mipango ya maendeleo katika maeneo yenu” amesema Mhe. Canoni
Mhe. Canoni amesema watendaji hao ni kiungo muhimu katika ya Serikali Kuu na Serikali za Mitaa hivyo wanapaswa kuwa wabunifu na kutoa ushauri wenye tija lakini pamoja na kuwatumia maafisa kama vile Maafisa Ugani wakati wa msimu wa kilimo na kujua utendaji wao wa kazi kwa manufaa ya wananchi na Taifa.
Aidha, Mhe. Canoni amewataka Watendaji wa Kata baada ya kuandaa mipango yao wahakikishe mipango yote ya maendeleo inapitia kwa Afisa Tarafa kabla ya kupelekwa kwa Mkurugenzi wa Halmashauri husika ili waweze kuwa na malengo ya pamoja.
Naye Ibrahimu Minja Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Tawala za Mikoa Ofisi ya Rais TAMISEMI amesema mafunzo hayo ya siku mbili yana lengo la kuwajengea uwezo watendaji hao ili waweze kufanya kazi zao kwa weledi ikiwa ni pamoja na ukusanyaji wa mapato, utatuzi wa migogoro na ushirikiano baina yao na wananchi.
Mafunzo hayo yamewezeshwa na Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa kutolewa mada mbalimbali ikiwa ni pamoja na Sera na Sheria zinazotumika katika Tawala za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa kujua mipaka ya utendaji kazi katika mamlaka hizo.