………………
CHAMA cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (TABOA) kimeipongeza Serikali kipitia Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (LATRA), kwa kuongeza viwango vya nauli huku kikipendekeza nauli hizo kuongezwa zaidi kwa madai ya gharama za uendeshaji kuwa juu.
Akizungumza Dar es Salaam ikiwa ni siku moja baada ya Latra kutangaza viwango hivyo vipya vya nauli, Msemaji wa Taboa Mustapha Mwalongo amesema pamoja na kuongezwa kwa viwango hivyo bado Latra inapaswa kuongeza nauli zaidi.
Amesema kolio chao hicho ni kutokana na kupanda kwa gharama za uendeshaji kwa kiasi kikubwa sambamba na kukua kwa mfumuko bei ambapo inawalazimu vipuri vingi kuwa juu huku vikinunuliwa kwa fedha ya kigeni dola ambayo kwa sasa gharama yake ya ubadirishaji kwa fedha ya hapa nchini imekuwa juu.
” Tunaaminj kupanda kwa viwango hivyo vya nauli kwa kiasi fulani kunakwenda kupunguza maumivu ambayo wasafirishaji wamekuwa wakikabiliana nayo lakini bado tunaiomba Serikali kuongeza viwango hivyo ili kutupunguzia makali” amesema Mwalongo
Amesema kwa kipindi kirefu sasa gharama za uendeshaji kwa vyombo hivyo muhimu kwa usafiri wa maelfu ya watanzania zimekuwa juu sambamba na kuboreshwa kwa huduma ya usafiri ambapo kwa sasa asilimia kubwa ya mabasi yanayotoa huduma ni ya kisasa.
Amesema tofauti na mabasi ya zamani kwa sasa mabasi mengi yanayotoa huduma ni mapya yakibeba abiria 37 hadi 50 huku yakiwa na huduma zote muhimu ikowemo kiyoyozi na mengine yakifungwa Televisheni.
“Pamoja na hayo kwa sasa tairi moja ambalo huko nyuma lilikuwa likiuzwa kwa Sh 400,000 bei yake imepanda hadi kufikia zaidi ya Sh 1000,000 ambali kuna vipuri vingine ambavyo navyo gharama zake zimepanda kwa kiasi kikubwa kiasi cha kutulazimu kuiomba Serikali kutuonea huruma ili kutokana na maumivu tunayoyapata” amesema Mwalongo.
Aidha amesema wao kama wasafirishaji wanaunga mkono jitihada zote zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali katika kuleta uwiano kwa kibiashara kwa kutangaza viwango vipya vya nauli pale ambapo gharama za uendeshaji zinapopanda ikiwemo ya nishati ya mafuta.
Ameiomba Latra kuangalia kwa kina pale pote walipogusia kuwa na mapungufu ili kuwawezesha kutoa huduma zao kwa ufanisi mkubwa akisisitiza kuwa Serikali ni sikivu na italisimamia suala hilo kwa umakini mkubwa.
Awali akitangaza kupandishwa kwa viwango hivyo vya nauli Jijini Arusha jana, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini(LATRA) CPA Habibu Suluo, ametangaza nauli hizo mpya kwa mabasi ya mijini (daladala) na masafa marefu (Mikoani na nchi za jirani)
Akitaja viwango hivyo amesema mabadiliko hayo yamefikiwa kwa kuzingatia sababu mbalimbali ikiwemo, uwezekano wa kuendelea kupanda kwa gharama za mafuta, kupanda kwa gharama za uwekezaji, maombi ya wasafirishaji na wamiliki wa mabasi pia kwa kurejea kifungu cha 21 cha Sheria ya Mamlaka ya Usafiri Ardhini, sura 413 pamoja na kanuni za Tozo za LATRA za mwaka 2020
“Nauli za safari zisizozidi kilometa 10 ambayo nauli ya awali ilikuwa Sh 500 sasa ni Sh 600, Safari za Kilometa 11 hadi 15, ilikuwa Sh 550 sasa itakuwa Sh 700.
Kilometa 16 hadi 20 nauli ilikuwa Sh 600 sasa itakuwa Sh 800. Safari za Kilometa 21 hadi 25 nauli kuwa Sh 700 hadi Sh 900.
Pia safari ya Kilometa 26 hadi 30 nauli itakuwa ni Sh 1100. Safari ya kilometa 31 hadi 35 nauli ya sasa ni Sh 10000 hivyo kupanda hadi Sh 1300 na kilometa 36 hadi 40 nauli ni 1400.” Amesema Suluo.
Amesema kwa upande wa nauli za wanafunzi hakuna mabadiliko, hivyo ni ile ile Sh 200 kwa daladala. Pia nauli za daladala ziandikwe ubavuni mwa daladala zao.
Aidha, Suluo amewaasa wasafirishaji na wamiliki wa vyombo kutotoza nauli kinyume na iliyotajwa na muongozo huo. Pia, kucheza nyimbo zisizo na maadili na mahubiri ya aina yoyote hayaruhusiwi
Suluo amesema yeyote mwenye hoja mbadala anaruhusiwa kukata rufaa ndani ya siku 14, vinginevyo hakuna kitakacho batilishwa.