NA SABIHA KHAMIS MAELEZO
Kamishna wa Jeshi la Polisi Zanzibar CP. Hamad Khamis Hamad amewataka viongozi wa Jeshi la Polisi kuwajibika kwa kufuata maadili ili kujenga imani kwa wanaowatumikia.
Akizungumza na viongozi Jeshi hilo wakati akifungua mafunzo ya maadili kwa viongozi wa umma huko Ziwani, amesema mafunzo hayo yatasaidia kuwajengea uwezo na uwelewa katika kutekeleza majukumu yao.
Amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uelewa viongozi wa Jeshi la Polisi juu ya kufuata maadili katika utendaji ili kupunguza wimbi la uhalifu na kuondoa hofu kwa raia.
Kamishna huyo ameeleza kuwa watumishi wakifuata vyema taratibu na sheria za utumishi wa umma katika uwajibikaji wao itasaidia kujenga msatakabali mzuri kwa jamii kwa kuijengea uaminifu na kuipa hadhi Jeshi la Polisi.
“Viongozi na watumishi tuwajibike katika kuutumikia umma, endapo maadili hayatofuatwa, imani ya wananchi kwa taasisi itashuka na kupelekea kushuka hadhi ya Taasisi” alisema Kamishna huyo.
Mapema Katibu Msaidizi wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Elizabeth Komba amesema Sekretarieti imepanga kuandaa mafunzo hayo kwa watumishi ili kuwakumbusha watumishi wa Jeshi la Polisi kutambua nafasi yao katika uwajibikaji na kuwa mfano katika jamii.
Amesema mafunzo waliyopatiwa viongozi hao yatasaidia kujiepusha na matumizi mabaya ya madaraka aliyonayo kwa kutoa maamuzi bila kuzingatia sheria na maadili ya utumishi na kwenda kinyume.
Nae mshiriki wa mafunzo hayo Kamishna Msaidizi wa Jeshi la Polisi kanda ya Mkoa wa Kaskazini Unguja RPC. Emanuel Samuel Shila amsema mafunzo hayo yatawasaidia kuzingatia maadali na umuhimu wa kuyatunza maadili hayo katika utekelezaji wa majukumu pamoja na kuitoa elimu kwa watumishi waliochini yao ili kulifikisha taifa mbele.
Mafunzo hayo ya siku moja yaliyotolewa kwa Jeshi la Polisi ambayo yameandaliwa na Sekretariti ya Maadili ya Viongozi wa Umma.