Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ushindani Tanzania (FCC) Bw. William Erio akizungumza leo Novemba 29, 2023 Jijini Dar es Salaam na waandishi wa habari wakati akizindua wiki ya ushindani.
…….
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Tume ya Ushindani Tanzania (FCC) imezindua wiki ya ushindani ambapo watatumia fursa hiyo kutoa elimu kwa wadau kutoka sekta mbalimbali nchini ikiwemo wafanyabiashara hasa kujiepusha na vitendo ambavyo vinarudisha nyuma ushindani na maendeleo ya Taifa.
Maadhimisho ya wiki ya ushindani ya mwaka 2023 yanaongozwa na kauli mbiu : Njama baina ya washindani na madhara yake kwa walaji na watumiaji, huku Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji anatarajiwa kuwa mgeni rasmi siku ya Kilele Disemba 5, 2023 Jijini Dar es Salaam.
Akizungumza leo Novemba 29, 2023 Jijini Dar es Salaam na waandishi wa habari wakati akizindua wiki ya ushindani, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ushindani Tanzania (FCC) Bw. William Erio, amesema katika kusherekea siku muhimu ya ushindani duniani Disemba 5 wameandaa semina kwa wadau mbalimbali katika kanda zote nchini.
Bw. Erio amesema kuwa katika wiki ya ushindani watakutana na wachimbaji wadogo wa madini kanda ya ziwa katika Mkoa wa Shinyanga kwa ajili ya kutoa elimu.
“Pia tutakutana na wazalishaji na wasambazaji wa mbegu za maua kanda ya kaskazini Mkoa wa Arusha, wakamuaji wa mchuzi wa zabibu, mafuta ya alizeti Mkoa wa Dodoma, Wafanyabiashara na wenye viwanda kutoka nyanda za juu Kusini Mkoa wa Mbeya pamoja na wakulima wa korosho Mkoa wa Mtwara” amesema Bw. Erio.
Amesema kuwa wadau wote watakaokutana nao watapewa elimu ya masuala ya kupanga njama pamoja na kujua mbinu ya namna ya kujiepusha na vitendo hivyo ambavyo vinarudisha nyuma maendeleo ya ushindani nchini.
Bw. Erio amesema kuwa FCC wana uwajibu kuwakumbusha wafanyabiashara kufanya biashara zao kwa kuzingatia kanuni na taratibu pamoja na misingi ya ushindani na kuwaelimisha wananchi kuhusu serikali yao nini inafanya katika kuhakikisha inawalinda.
Amefafanua kuwa siku ya ushindani duniani imelenga kuelimisha jamii, wadau kutoka sekta mbalimbali kuhusu kuzingatia umuhimu wa kanuni za biashara.
“Kanuni za biashara zinawafanya watendaji wa biashara kuwa na fursa sawa kwa wote, na sheria zetu zipo katika mambo kadhaa ambayo yanazuia na vitu ambavyo vitarudisha maendeleo ya kufanya biashara” amesema Bw. Erio.
Amesema kuwa vitu ambavyo sheria inakataza ni pamoja na kupanga bei za bidhaa wanazofanya, kupunguza uzalishaji, kugawana zabuni pamoja na kula njama ambayo itapelekea kurudisha nyuma maendeleo ya ushindani.
Miongoni mwa majukumu ya FCC ni kuongeza ufanisi katika uzalishaji, usambazaji na ugavi wa bidhaa na huduma katika kuhakikisha mazingira sawa ya ushindani wa soko baada ya nchi kuondokana na mfumo wa uchumi hodhi na kuhamia katika mfumo wa uchumi wa soko huria kwa maslahi mapana ya Taifa.