Na Sixmund Begashe
Wizara ya Maliasili na Utalii imeihakikishia Benki ya Dunia kuwa itaendelea kusimamia vyema utekelezaji wa Mradi wa Kuboresha Usimamizi wa Maliasili na Kukuza Utalii Kusini mwa Tanzania na namna wananchi wanavyo shirikishwa vyema kwenye utekelezaji wa mradi huo.
Hayo yamesemwa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii Kamishna Benedict Wakulyamba mkoani Morogoro, alipokuwa akifungua kikao kazi cha pamoja kati ya wataam kutoka Benki ya Dunia na watekelezaji wa mradi kwa lengo la kupata uelewa wa pamoja wa hatua zilizofikiwa za utekelezaji wa mradi.
Kamishna Wakulyamba amesema kuwa, pongezi zilizotolewa na Benki ya Dunia kwa Serikali ya Tanzania kwa juhudi inazozifanya katika kutekeleza Mradi kwa kasi, ni matokeo chanya ya jitihada za Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Mhe Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuinua sekta ya Utalii kiuhifadhi na Utalii nchini kwa maslai mapana ya Taifa kwa ujumla.
Aidha Kamishna Wakulyamba ametoa wito kwa wakandarasi wote wanaotekeleza mradi wa REGROW kuhakikisha wanakamilisha ujenzi wa miradi hiyo kwa wakati uliopangwa na kwa ubora, na wananchi kuunga mkono juhudi hizo za Serikali kwa kutoungana na watu wachache wenye nia ya kukwamisha utekelezaji wa mradi kwa kuwa nia yao ni kuvuruga mpango wa Serikali wa kuwaletea wananchi maendeleo.
Akizungumza kwenye kikao hicho, Msimamizi Mkuu wa Mradi wa REGROW wa Benki ya Dunia Dkt. Enos Esikuri amesema wameridhishwa na hatua zilizofikiwa za utekelezaji wa Mradi huo, na kuwa Benki ya Dunia itaendelea kufuatilia kwa ukaribu sehemu iliyobaki ambayo inaendelea kutekelezwa ili kuhakikisha taratibu zote zilizopo zinafuatwa na hatimae Mradi utakapokamilika watanzania wanufaike kwa uhifadhi endelevu na ongezeko la mapato ya nchini kupitia sekta ya Utalii.
Dkt. Esikuri ameongeza kuwa Tanzania imejaliwa kwa utajiri mkubwa wa Maliasili na vivutio vya kipekee, hivyo utekelezaji wa mradi wa REGROW si kwa manufaa tu ya Tanzania bali ni kwa faida ya Afrika kwa ujumla huku ikikumbukwa kuwa mradi huo unatekelezwa pia kwenye Hifadhi kubwa kuliko zote Afrika, Hifadhi ya Taifa Nyerere ambayo ni Urithi muhimu kwa waafrika.