Makamo Mwenyekiti wa Tume ya haki za Binaadamu na Utawala Bora Mohammed Khamis Hamad akizungumza na Waandishi wa Habari juu ya kitendo cha udhalilishaji wa Hashim Ally Philemon unaodaiwa kufanywa na Mbunge wa Babati Mjini Pauline Philipp Gekul. (PICHA NA FAUZIA MUSSA –MAELEZO ZANZIBAR)
NA SABIHA KHAMIS MAELEZO
Tume ya Haki za Binaadamu na Utawala Bora (THBUB) imekusudia kufanya uchunguzi wa kina kutokana na tuhuma za ukatili na udhalilishaji unaodaiwa kufanywa na Mbunge wa Babati Mjini Mhe. Pauline Philipo Gekul dhidi ya Bw. Hashim Ally Phillemon mkaazi wa Babati Mjini.
Akizungumza na Waadishi wa Habari katika ukumbi wa Studio Raha leo Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binaadam na Utawala Bora Mohaned Khamis Hamad amesema taarifa za kitendo hicho zimekuwa zikisambaa katika vyombo mbalimbali vya habari na mitandao ya kijamii hivyo tume imeamua kufuatilia kwa kina ili kupata usahihi wa taarifa hizo.
Amesema pamoja na hatua zilizochukuliwa na Mamlaka mbali mbali (THBUB) imeona kuna haja ya kufanya uchunguzi huo kwa mujibu wa ibara ya 130 (1) (c) na (f) ya Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 1977 na kifuungu cha 6 (1) c, f, g pamoja na kifungu cha 15 (1) (a) vya Sheria ya THBUB sura ya 391 ili kubaini ukweli wa tuhuma hizo.
Aidha, amesema Bw. Hashim Ally Phillemon alikamatwa na kujeruhiwa sehemu mbali mbali katika mwili wake akiwa katika mazingira ya kazini kwake jambo ambalo limepelekea kupata maumivu makali katika mwili wake.
“Kama inavyoelezwa na vyombo vya habari kwamba Bw. Hashim Ally Phillemon alikamatwa, kupigwa, kujeruhiwa na kuwekewa chupa katika eneo la haja kubwa akiwa kazini kama mtumishi wa Paleii Lake View Garden, inayodaiwa kumilikiwa na Mbunge huyo” alisema Makamu Mwenyekiti.
Hata hivyo ameeleza kuwa chanzo cha udhalilishaji huo kinadaiwa kuwa ni kutumwa na mshindani wa kibiahara wa Mbunge huyo kumuwekea sumu na kumuua.
Tuhuma hizo ziliibuka Novemba 25, 2023 baada ya kusambaa kwa video mitandaoni ikimuonesha Bw. Hashim Ally Phillemon akielezea ukatili na udhlilishaji aliofanyiwa na Mbunge huyo.