Kamishna wa Idara ya Uchambuzi wa Sera, Wizara ya Fedha, Bw. William Mhoja, akieleza kuhusu umuhimu wa maoni ya wananchi katika uboreshaji wa Sera za Kodi wakati wa Kongamano la kukusanya maoni ya Kodi Kikanda lililofanyika mkoani Kigoma, ikiwa ni mwendelezo wa makongamano hayo ya uboreshaji wa Kodi. Kushoto ni Meneja Huduma wa Taasisi ya Usuluhishi wa Malalamiko na Taarifa za Kodi (TOST), Bw. Godwin Barongo na Kulia ni Afisa Biashara Mkoa wa Kigoma Bw. Moshi Ndimuligo.
Meneja Huduma wa Taasisi ya Usuluhishi wa Malalamiko na Taarifa za Kodi (TOST), Bw. Godwin Barongo, akieleza malengo ya kuanzishwa kwa Taasisi hiyo ikiwa ni pamoja na kutatua malalamiko ya Kodi, wakati wa Kongamano la kukusanya maoni ya Kodi Kikanda lililofanyika mkoani Kigoma. Kulia ni Kamishna wa Idara ya Uchambuzi wa Sera, Wizara ya Fedha, Bw. William Mhoja.
Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara, Viwanda na Kilimo (TCCIA) Mkoa wa Kigoma, Bw. Shabani Yabulula, akitoa maoni kuhusu uboreshaji wa Sera ya Kodi wakati wa Kongamano la kukusanya maoni ya Kodi Kikanda, lililofanyika mkoani Kigoma.
Katibu wa Chemba ya Wanawake Wafanyabiashara Mkoa wa Kigoma, Bi. Chichi Kamandwa, akitoa maoni kuhusu Kodi ili kuboresha Sera ya Kodi kwa mwaka 2024/25, wakati wa Kongamano la kukusanya maoni ya Kodi Kikanda lililofanyika mkoani Kigoma.
Mwenyekiti wa Wamiliki na Wasafirishaji Maboti Mkoa wa Kigoma, Bw. Kashindi Adamu, akieleza kuhusu maboresho ya kodi kwenye sekta ya Usafirishaji kwa mwaka 2024/25, wakati wa Kongamano la kukusanya maoni ya Kodi Kikanda lililofanyika mkoani Kigoma.
Meneja wa Chemba ya Kilimo mkoa wa Kigoma, Bw. Selestin Nestory, akiwasilisha mada kuhusu maoni ya maboresho ya Kodi kwa mwaka 2024/25, wakati wa Kongamano la kukusanya maoni ya Kodi Kikanda lililofanyika mkoani Kigoma.
Kiongozi wa Wasafirishaji Mkoa wa Kigoma, Bw. Soud Ahmad, akieleza kuhusu maboresho ya kodi kwenye sekta ya Usafirishaji kwa mwaka 2024/25, wakati wa Kongamano la kukusanya maoni ya Kodi Kikanda linalofanywa na Wizara ya Fedha na wadau wengine, mkoani Kigoma.
Kamishna wa Idara ya Uchambuzi wa Sera, Wizara ya Fedha, Bw. William Mhoja na wadau wa kodi mkoa wa Kigoma wakiwa katika picha ya pamoja na Timu ya Ukusanyaji maoni ya Kodi kutoka Wizara ya Fedha na Sekta binafsi, baada ya Kongamano la ukusanyaji maoni ya utozaji kodi kwa mwaka 2024/25, mkoani Kigoma.
………………………..
Na. Peter Haule, WF, Kigoma
Serikali inakusanya maoni ili kuboresha Sera ya uutozaji kodi kwa mwaka 2024/25 kwa kuhusisha makundi mbalimbali kwenye Sekretarieti ikiwemo Sekta binafsi ili kuwa na Sera madhubuti yenye kukidhi kwa kiasi kikubwa mahitaji ya wadau wa kodi nchini.
Hayo yameelezwa na Kamishna wa Idara ya Uchambuzi wa Sera, Wizara ya Fedha, Bw. William Mhoja, wakati wa Kongamano la ukusanyaji maoni ya Kodi Kikanda mkoani Kigoma, ikiwa ni muendelezo wa makongamano kama hayo yanayofanyika Kanda mbalimbali nchini kwa lengo la kuboresha Sera ya Kodi kwa mwaka 2024/25.
Alisema kuwa Timu ya Wataalamu wa ukusanyaji maoni imeshirikisha pia Sekta binafsi eneo la Viwanda, Chama cha Wafanyabiashara, Viwanda na Kilimo (TCCIA), sekta ya Viwanda, Biashara, Mifugo na Uvuvi.
“Maoni yanayoendelea kutolewa yana maudhui yanayohitajika katika kuboresha Sera, ambapo yatachukuliwa na kuchakatwa ili kuangalia ufanisi wake katika maendeleo ya watu na nchi kwa ujumla bila kuathiri matokeo ya kodi katika kupeleka huduma bora kwa wananchi zikiwemo za Afya, Miundombinu ya Barabara, nishati na maji’’, alisema Bw. Mhoja.
Aidha, aliwataka wananchi wa Mkoa wa Kigoma kuzitumia Taasisi zilizopo mkoani hapo kupata majibu ya mambo mbalimbali kwa kuwa zipo kero ambazo zinazungumzwa na wananchi ili hali zilitafutiwa ufumbuzi na taratibu na Sheria zilibadilishwa.
Pia Kamishna Mhoja alitoa rai kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania kuendelea kutoa elimu kwa wananchi ili kujua jitihada ambazo Serikali imezifanya katika kurekebisha kodi mbalimbali kwa manufaa ya wananchi wake ikiwa ni pamoja na adhabu za kutopokea risiti ambapo aliyetenda kosa anatakiwa kulipa faini asilimia 20 ya kodi ambayo alitakiwa kulipa ikiwa angechukua risiti.
Kwa upande wake Meneja Huduma wa Taasisi ya Usuluhishi wa Malalamiko na Taarifa za Kodi (TOST), Bw. Godwin Barongo, alisema kuwa, Taasisi hiyo imeanzishwa ili kutafuta suluhisho ya malalamiko ambayo hayajapatiwa ufumbuzi na Mamlaka ya Mapato Tanzania lakini haina madhumuni ya kuwafanya watu wasilipe Kodi.
Alisema kuwa tayari Taasisi hiyo imeanza kupokea malalamiko kutoka mikoa mbalimbali ikiwemo Kigoma na wanayafanyiakazi, alieleza kuwa malalamiko yanaweza kuwafikia kwa njia ya simu au kufika ofisini moja kwa moja bila kutozwa gharama yoyote.
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara, Viwanda na Kilimo (TCCIA), mkoa wa Kigoma alisema kuwa wakati maoni ya utozaji kodi yakiendelea kutolewa na kufanyiwa kazi kwa mwaka wa fedha 2024/25, ameiomba Serikali kuendelea na jitihada za kuondoa vikwanzo vya ufanyaji biashara kwa upande wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, ili kuimarisha biashara kati ya nchi hizo mbili.
Timu ya Wataalam wa Uchambuzi wa Sera za Kodi kutoka Wizara ya Fedha ianendelea na ukusanyaji wa maoni kwa wananchi Kikanda ambapo hadi sasa mkoa wa Arusha, Mwanza na Kigoma imefikiwa.