Na Issa Mwadangala
Askari Polisi nchini wametakiwa kuwa na matumizi mazuri na sahihi ya rasilimali vifaa vinavyotolewa na serikali katika jitihada za kuendelea kutoa elimu kwa wananchi dhidi ya mapambano ya uhalifu.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Songwe Mhe. Dkt. Fransis Michael, Novemba 28, 2023 wakati akikabidhi pikipiki nane kwa Wakaguzi wa Polisi ambao ni Polisi kata katika kata zilizopo mkoani Songwe, pikipiki ambazo zimetolewa kwa lengo la kurahisisha usafiri wa kuyafikia maeneo mbalimbali kutoa elimu kwa wananchi kuhusu athari za uhalifu na unyanyasaji wa kijinsia.
Kwa upande wake Kamanda wa Polisi mkoa wa Songwe Kamishna Msaidizi wa Polisi ACP Theopista Mallya, ameishukuru serikali ya awamu ya sita kwa kuendelea kutoa vitendea kazi kwa Jeshi la Polisi jambo lililopelekea Jeshi la Polisi mkoani Songwe kufaidika na vifaa hivyo yakiwemo Magarina Pikipiki.